Tanzania tunahitaji Mwakinyo wengine

30Nov 2019
Mhariri
Nipashe
Tanzania tunahitaji Mwakinyo wengine

WAKATI jana usiku, bondia wa ngumi za kulipwa nchini, Hassan Mwakinyo, alikuwa anapanda jukwaani kupambana na mpinzani wake, Arnel Tinampay, kutoka Filipino, huu ni wakati mwingine wa kukumbuka kuzalisha mabondia wengine.

Mwakinyo anaonekana kufanya vizuri baada ya kupata udhamini kutoka katika kampuni mojawapo ya michezo ya kubahatisha hapa nchini.

Kwa muda mrefu, Tanzania ilikuwa imepotea kwenye medani na ushindani wa kimataifa katika mchezo wa ngumi, lakini kupitia bondia huyo kutoka jijini Tanga, tumeanza kupeperusha bendera yetu.

Hata hivyo, Mwakinyo, ambaye kwa Afrika anashikilia nafasi ya kwanza, kama walivyo wanamichezo wengine ambao wanafanya vema kimataifa, amepata umaarufu kutokana na jitihada zake binafsi.

Bondia huyo alianza kujifua kwa kutumia vifaa vya "mtaani", lishe ya kubahatisha, lakini leo hii Watanzania tunajivunia kutokana na nafasi ambayo amefikia katika mchezo huo.

Wadau wa michezo ambao wanaongozwa na serikali, taasisi na kampuni mbalimbali, huu ndio muda sahihi wa kuwekeza katika mchezo huo kwa kusaidia maandalizi, kuleta makocha wenye uzoefu na kuwanunulia vifaa vya kisasa mabondia chipukizi ambao wameonyesha kuwa na vipaji.

Kamwe tusisubiri mpaka Mwakinyo 'apotee", huku kutakuwa si kusaidia maendeleo ya michezo na inatakiwa kutumia jina la bondia huyo kuendesha mafunzo mbalimbali ya kuwaendeleza mabondia chipukizi kutoka mikoa yote hapa nchini.

Imetuchukua muda mrefu Watanzania kupata bondia ambaye anafanya vema katika mapambano ya kimataifa, tangu zama za Rashid Matumla 'Snake Boy" na Maneno Oswald 'Mtambo wa Gongo" kustaafu mchezo huo, wakiwa na mikanda mbalimbali ya kitaifa na kimataifa ambayo waliichukua.

Nipashe tunasema kuwa, kama tunavyoshuhudia katika upande wa soka, wakati kiwango cha nahodha wa Timu ya Taifa (Taifa Stars), Mbwana Samatta, ambaye anacheza soka la kulipwa katika klabu ya KRC Genk inayoshiriki Ligi Kuu Ubelgiji, kikiwa bado juu, tayari wachezaji wengine wanafanya vema kwenye klabu za nje akiwamo Simon Msuva na Abdallah Yusuph.

Tunashuhudia mshambuliaji chipukizi, Kelvin John, tayari ameshafanya majaribio katika klabu mbalimbali za Ulaya, na hii inamaanisha kwamba wataungana mapema kupeperusha bendera ya Tanzania kwa kucheza soka la kulipwa sambamba na Samatta.

Hali hii ndio tunataka kuiona pia katika mchezo wa ngumi, kwa Mwakinyo, kuwavuta mabondia wengine hali ya kuwa yeye bado anafanya vema kwenye mashindano ya kimataifa anayoshiriki.

Kuandaa wanamichezo chipukizi, ndio siri pekee ambayo itatufanya Watanzania kuwa na mabondia wengi watakaokuwa wanapambana mara kwa mara na kuacha kutegemea kumuona bondia mmoja akishiriki mashindano mbalimbali.

Endapo tutafanikiwa kuwa na mabondia wengi wenye viwango vinavyofanana na Mwakinyo, inamaana bendera ya Tanzania itakuwa ikipeperushwa katika mashindano mengi zaidi, lakini pia mchezo huo ukiendelea kutoa ajira kwa vijana hao pamoja na makocha wao.

Njia hii ndio itatufanya tung'are zaidi katika medani za kimataifa, kwa sababu tunaamini mafanikio yoyote kwenye michezo, hayawezi kupatikana kwa miujiza, ila kwa kuwa na maandalizi sahihi ambayo yanaanzia katika kuwapa mafunzo mabondia chipukizi.

Habari Kubwa