Atangaye sana na jua hujua

30Nov 2019
Barnabas Maro
Nipashe
Atangaye sana na jua hujua

KUTEMBEA kwingi ni kujua mengi kwa kuwa mtu anaishia kukusanya maarifa mengi. Methali hii yatunasihi tutembee na kujifunza mengi.

Mpira wa miguu ni kati ya michezo inayopendwa sana duniani. Huitwa kabumbu, kandanda, soka na gozi. Ili kuupamba zaidi mchezo huo, wengine husema ‘gozi la ng’ombe nyama kala nani?’

Ni mchezo wenye fadhaa yaani hali ya wasiwasi; jakamoyo. Hali ya mtu kupatwa na m-babaiko kutokana na jambo la kushtua.

Mchezo huo huvuta maelfu ya watazamaji wanaojaza viwanja hasa kwa hapa nchini, zinapocheza timu mbili zenye mvutano mkubwa, Simba na Yanga.

Nimeona baadhi ya wanachama au mashabiki walioahidi kutoa wake zao endapo timu zao zitashindwa! Sasa naelewa ni kwa nini wahenga walisema “Kipendacho moyo ni dawa.”

Maana yake kitu anachopenda mtu au inachopenda roho ya mtu huwa ni kama dawa yake. Methali hii yaweza kutumiwa kumpigia mfano mtu anayeelekea kukipenda kitu fulani sana ingawa wengine wanakiona kuwa kibaya.

Kinachowaangusha watazamaji uwanjani na kuzirai zichezapo Simba na Yanga ni kitu gani? Ni ahadi zilizotolewa na wanachama, wapenzi na mashabiki wa timu hizo kuwa moja ‘lazima’ ishinde na kama ikishindwa, basi atakuwa radhi kutoa kitu alichoahidi kumpa mpinzani wake!

Baadhi ya mashabiki wa timu hizo hupandwa na mizuka (mapepo) timu zao zinaposhinda au kushindwa!

Nakumbuka miaka ya ’60 pale Magomeni Mapipa palipokuwa na mzunguko, kuna shabiki wa Simba aliyekesha juu ya mti baada ya timu yake kuishinda Yanga!

Ni nadhiri aliyojiwekea endapo Simba ingeishinda Yanga na alitimiza. Kumbe ndo maana wahenga walisema: “Ahadi ni deni na deni ijuzie.” Maana yake ahadi ni kama deni, mtu akitoa ahadi lazima aitimize. Methali hii yatufunza umuhimu wa kutimiza ahadi tutoazo.

Ni wakati Yanga ilipokuwa ikiitesa sana Simba kila zilipokutana kwenye uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam.

Vimuyemuye (wasiwasi, wahaka) vya Simba na Yanga vilikuwepo tangu zamani. Kwenye makutano ya barabara za Mafia na Msimbazi, kabla ya timu hizo kucheza, walikuwepo wanachama wa pande zote mbili.

Kila mmoja alitokosa majani kwenye chungu chake huku bendera zao zikipepea mbele. Chini kuliwekwa sinia kubwa kila upande ili wanachama na mashabiki waweke kiasi chochote cha hela. Jambo hilo lilifanyika bila kutukanana, kusukumana wala kuoneana wivu kwa upande uliokusanya fedha nyingi zaidi.

Simba ilipoishinda Yanga, kombe lilizungushwa jiji zima la Dar es Salaam hata kupita nje ya klabu ya Yanga na mashabiki kutumbukiza kiasi chochote cha hela ndani ya kombe. Kadhalika ilikuwa vivyo hivyo Yanga ilipoishinda Simba na kutwaa kombe.

Siku hizi timu hizo zachukiana mithili ya m-mbwa na paka! Hakuna yoyote inayothubutu kupita na kombe la ushindi mbele ya klabu ya mwingine. Kinachosemwa ‘utani wa jadi’ kimepitwa na wakati kwani sasa ni ubaya ubaya tu!

Uhasama huo umesababisha hata timu ngeni inapokuja kucheza na Simba au Yanga, kupokewa na moja ya timu hizi na kuwapa siri zote za Simba au Yanga!

Kwa vile ‘wajinga ndiwo waliwao,” timu ngeni huja na jezi zenye rangi za Simba na Yanga, nasi kwa uzuzu (uwezo mdogo wa kufahamu mambo; hali ya mtu kutolijua jambo linaloendelea) wetu huzinunua na kuzivaa siku ya mechi huku tukizishangilia timu ngeni!

Kama Simba na Yanga ni ya Watanzania, kwa nini tufanyiane uhasama? Upendo ule wa zamani u’wapi? Kwa nini tuchukiane ili kuwafurahisha wageni? Hatujui tunajidharau na kujitukana wenyewe!?

Mbona zamani tulikuwa waungwana (watu tunaojistahi, wenye tabia inayokubalika katika jamii) lakini sasa tumekuwa watwana (wanaume wanaomilikiwa na watu wengine na kufanyishwa kazi bila ujira) wenyewe kwa wenyewe?

Siku hizi mpenzi au mwanachama wa Yanga kukaa upande wa Simba au mpenzi wa Simba kukaa upande wa Yanga atajuta kuzaliwa.

Kule kuvaa jezi ya Simba ukaonekana umekaa upande wa Yanga au kuvaa jezi ya Yanga ukaonekana upande wa Simba ni kitimbi (kitendo cha hila kinachotendwa dhidi ya mtu mwingine; kitendo cha kuchekesha au kumdhalilisha mtu)!

Nakumbuka zamani, nikiwa na mwenzangu tulikwenda kuangalia mechi ya Simba na Yanga. Kwa kuwa upande wa Yanga ulifurika pomoni (katika hali ya kujaa au kuwa –ingi) tulikwenda kukaa jukwaa la Simba.

Simba ilikuwa ya kwanza kuifunga Yanga tena kwa bao la mapema. Wenzetu wakaruka kushangilia huku sisi tukijikunyata kama tuliomwagiwa maji ya baridi sana. Mwenzangu akaniambia: “Tulia watanyamaza sasa hivi.”

Baada ya muda mfupi Yanga wakasawazisha nasi tukaruka kushangilia bao lile. Dakika kumi baadaye Yanga ikafunga bao la pili na la ushindi na kutufanya turukeruke sana na kushangilia.

Ingawa tulikuwa upande wa Simba, hakuna yeyote aliyetufukuza. Ingekuwa siku hizi, tungenyanyuliwa, kutukanwa, kupigwa na kutupiwa upande wa Yanga!

Kwa nini tumeuacha uungwana ule? Tujitathmini.

Habari Kubwa