Aliyehitimu kwa bango kubwa Udom afunguka

30Nov 2019
Augusta Njoji
DODOMA
Nipashe
Aliyehitimu kwa bango kubwa Udom afunguka
  • *Baba yake anamiliki shule ya sekondari
  • *Awa mkurugenzi, amponza mama yake

ALIKUWA anasomea kijiji? Ni wa kwanza kwao kupata shahada?, Ni baadhi ya maswali ambayo wengi walihoji baada ya kuona picha ya bango kubwa la kuhitimu chuo kikuu kwa Ayubu Malambugi.

Ayubu Malambugi akipozi kwa picha katika mahafali.

Picha ya Ayubu, mhitimu wa Shahada ya Sanaa na Elimu katika Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) mwaka huu, ilisambaa kwa kasi kwenye mitandao ya kijamii wiki iliyopita kutokana na upekee wake.

Ilikuwa picha yenye bango kubwa lililoandaliwa kwa ustadi, likiwa na maneno ya kumpongeza kwa kupata shahada hiyo Novemba 22, mwaka huu, Malambugi akiwa miongoni mwa wahitimu 5,425 wa shahada ya kwanza katika chuo hicho.

Bango hilo lilikuwa na maneno yaliyosomeka ‘Hongera Ayubu N. Malambugi kwa kuhitimu na kupata shahada ya kwanza ya elimu Chuo Kikuu cha Dodoma' na limempa umaarufu kijana huyo.

SAFARI YAKE KIELIMU

Nipashe ilimtafuta Ayubu ili kujua safari yake kielimu na sababu ya kuwapo kwa bango hilo kwenye mahafali yake.

Anasema kidato cha kwanza hadi cha nne alisoma katika Shule ya Sekondari Airport mkoani Mbeya ambayo inamilikiwa na baba yake, Nikuswiga Malambugi.

“Nilisoma pale kwa miaka minne kuanzia mwaka 2010 hadi 2013. Nilipohitimu kidato cha nne, nilifanikiwa kufaulu na kuchaguliwa shule ya serikali kwa ajili ya kidato cha tano na sita iitwayo Kiwanja, ipo wilayani Chunya. Nilihitimu pale mwaka 2016.

“Sikupata matatizo yoyote shuleni kwa upande wa walimu na wanafunzi wenzangu, ninamshukuru Mungu nilimaliza salama, nikafanikiwa kufaulu na wakati wa kujiunga na chuo kikuu, nikachaguliwa kujiunga na Udom," anasema.

BANGO KUBWA

Ayubu alisema bango lililompa umaarufu mkubwa kwenye mitandao ya kijamii, lilitengenezwa na baba yake na ilikuwa zawadi ya kushtukiza kwake.

“Ilikuwa kama 'surprise' (ya kushangaza) kutoka kwa baba, wanafamilia wote waliokuja Chimwaga kwenye mahafali, japo walitoka Mbeya na mzee mpaka Dodoma kwa gari lake, hakuna aliyejua kuwa ameandaa lile bango kubwa," anasema.

Ayubu anadai baba yake ni mbunifu na mara nyingi huwa si rahisi kuelewa kitu anachoandaa hadi kinapokamilika.

“Hili bango nilipewa baada ya kutoka ukumbini Chimwaga kwenye sherehe za kutunukiwa, baba akatuambia wote tulipofika nje kuwa ameniandalia 'surprise'.

"Tulipofika karibu na gari lake, akatusimamisha halafu yeye akaenda kuchukua hilo bango ikawa 'surprise' kweli kweli kwa wote tuliokuwapo, tukafurahi na tukaanza kupiga nalo picha,” anasema.

Mhitimu huyo anasema alifurahi na kufarijika kutokana na ubunifu wa baba yake, akieleza kuwa imempa motisha ya kufanya vizuri zaidi katika mipango yake kimaisha.

“Nilijisikia vizuri sana na tulifurahi pamoja pale familia nzima kwa sababu najua baba yangu ni 'creative' kinoma kwa mambo anayofanya," anasifu.

Ayubu anabainisha kuwa sasa anakumbana na utani mwingi hasa kwenye mitandao ya kijamii kutokana na kubamba kwa bango lake hilo.

“Mimi nauchukulia poa, mpaka rafiki zangu kwa sasa wananiita 'bango kubwa'.“Baada ya kurudi nyumbani Mbeya, familia ilirudi Jumamosi, mimi nilirudi Jumatatu, baba akaniambia kuwa hakutarajia na hakufikiri suala hilo lingekuwa kubwa na kusambaa kwa kiwango kikubwa kwenye mitandao ya kijamii.

"Mimi kwa kweli sikutegemea, nilipatwa na mshangao mkubwa, niliona ni kitu cha kipekee sana mzee kafanya. Ndani ya zile sekunde za kwanza niliwaza kweli kuwa hii watu wataona kitu cha ajabu sana.

"Lakini, katika maisha yangu, sijawahi kuwaza ya walimwengu watasema nini, mimi nilipokea kwa furaha sana kutoka kwa baba na tulicheka sana," anasema.

APEWA UKURUGENZI

Ayubu anaeleza kuwa baada ya kuhitimu, ameungana na baba yake kusaidia utekelezaji wa majukumu ya uendeshaji wa shule na amepewa nafasi ya kuwa msaidizi wake, akiitwa mkurugenzi mdogo.

“Mimi ni mtoto wa tano kwa baba, walio juu yangu wawili wameajiriwa serikalini, tofauti na wengine wanavyotafsiri lile bango kwenye mitandao wakidhani labda mimi ndiyo mhitimu wa kwanza kwenye familia yetu, wapo wasomi wengine," anasema.

"Jambo la kuumiza ni kwamba, baba yangu ni mkali sana. Wiki moja kabla ya mahafali, aliniambia ninyoe ndevu maana nilikuwa nimeachia ndevu, zikawa nyingi. Sasa baba hapendi mtu afuge nywele na ndevu, yeye anaona ni uchafu.

“Sasa, mimi aliponiambia ninyoe ndevu nikamwambia nitanyoa mahafali ikipita, nikawa nimemchokoza, akasema hata mahafali yangu hatahudhuria, niliomba msamaha akakataa.

"Mama akanisaidia lakini akaambia 'wewe hujamfunza adabu', kitendo kile kiliniuma sana, lakini baadaye alinisamehe kwa sababu si unajua mtoto ni mtoto tu," anasema.

Ayubu anakiri kufanikiwa kwake kitaaluma kumetokana na usimamizi mzuri wa wazazi wake, akishauri wazazi kuwajengea msingi mzuri watoto wao kielimu kwa kuhakikisha wanafuatilia maendeleo ya watoto taaluma badala ya kuacha jukumu hilo kwa walimu.

NDOTO YAKE

Anasema licha ya baba yake kujikita katika taaluma anakomsaidia, ndoto yake ni kuwa mfanyabiashara mkubwa nchini.

"Malengo yangu ni kuwa mfanyabiashara. Niwe na miradi mbalimbali ambayo itaniingizia fedha nyingi huku nikiendelea kupiga kazi na baba hapa Airport High School Mbeya,” anasema.

MARAFIKI WANENA

Kiongozi wa darasa alilokuwa anasoma Ayubu, Ismail Haji, anasema kijana huyo alikuwa anafahamika kwa mambo mawili, mwanamichezo na mtu aliyekuwa akishiriki vyema kwenye majadiliano ya masomo na wenzake.

“Ayubu alikuwa kocha msaidizi wa kikosi chetu na tulifanikiwa kuchukua ubingwa kwenye idara yenu ya Arts Media and Designing.

"Nilipoona lile bango, nilikuwa nataka kujua ni nani aliyempatia au alitengeneza mwenyewe maana ni mcheshi sana," Haji anasema.

Anaeleza kuwa bango hilo lilimpa funzo kwamba, bado kuna wazazi wanaopenda kutoa motisha kwa watoto wao ili wafanye mambo makubwa zaidi.

“Kuna wengine wanatoa zawadi fulani kama motisha kwa mhitimu kutokana na mazingira ambayo ametoka, wengine wanatoa zawadi kama ile.

"Kimsingi, kila mtu anachukulia kwa uzito wake, mzazi wake alitaka kuonyesha umma wa Udom kwamba mzazi amefurahishwa na hatua hiyo," anasema.

Mwalimu Yohana Mwalusambo anayefundisha katika shule ya baba yake, anasema bango hilo ni motisha iliyotolewa na mzazi kwa mtoto kwa kuhitimu shahada ya kwanza.

“Hii sisi kama walimu tuliona ni suala kama motisha, yalizungumzwa mengi kuhusu picha yake, iliibua mijadala mitandaoni kwa kuwa ni nadra kufanyika kwa mhitimu wa chuo kikuu.

"Wapo waliosema anasomea kijiji, wengine wakasema ni mhitimu wa kwanza wa familia, kumbe si kweli. Bango lile ilikuwa ni kama kutambua kuwa amehitimu masomo yake,”anasema.

Andrew Malambugi ambaye ni kaka wa Ayubu, naye anakiri kushangazwa na bango la baba yao, akieleza kuwa hakutarajia kama mzee wao angeibuka na kitu hicho.

"Kiukweli, lile bango lilikuwa 'surprise' kwetu, lakini baba yenu ni mbunifu, huwa anatumia akili kubwa kufikiria kitu cha tofauti ambacho hata mtu mwingine akiona, anaanza kushangaa," anasema.

"Tulipoona jambo hilo linasambaa kwa kasi mitandaoni, tulishtuka lakini tulichukulia kawaida maana watu hawajazoea kuona bango la aina hiyo kwenye mahafali ya chuoni.

"Kuna watu walihisi Ayubu ni wa kwanza kuhitimu chuo kikuu katika familia yetu, lakini siyo kweli, Ayubu ni wa nne kwa watoto wa mzee kuhitimu chuo kikuu, wengine wawili wapo vyuo vikuu, wengine waliobaki wako sekondari na msingi. Kwa kifupi, familia yetu wote wameenda shule," alisema.

Habari Kubwa