Simbachawene, Jafo waanika fursa mradi wa Mto Msimbazi

30Nov 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Simbachawene, Jafo waanika fursa mradi wa Mto Msimbazi

UELEWA zaidi juu ya mradi wa ujenzi wa Mto Msimbazi jijini Dar es Salaam unatakiwa kutolewa ili mradi huo ufanikiwe.

Kauli hiyo ilitolewa jana jijini na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, George Simbachawene, wakati wa kikao cha kupokea wasilisho la mpango wa fursa za uwekezaji katika bonde la mto huo na suluhisho la kudumu la mafuriko katika jiji hilo.

“Mradi huu ni muhimu sana na uchambuzi wa kina unahitajika pamoja na uelewa zaidi ili kukamilisha mradi huu, na kila mmoja anatakiwa kuona umuhimu wa mradi huu," alisema.

Katika kikao hicho, Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Seleman Jafo, alisema mradi huo ni fursa ya uwekezaji katika Jiji la Dar es Salaam na ukifanikiwa, mandhari ya jiji hilo itapendeza na kuwa kivutio cha utalii.

Kikao hicho kiliandaliwa na Simbachawene, ikiwa ni maelekezo ya Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, aliyotoa ili kutafuta suluhu ya kudumu ya mafuriko katika Jiji la Dar es Salaam na kukabiliana na madhara yanayosababishwa na mafuriko.

Mawaziri wengine waliotakiwa kushiriki katika upokeaji wa wasilisho hilo ni Waziri wa Fedha na Mipango, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Waziri wa Maji na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambao waliwakilishwa na maofisa kutoka wizara zao.

Habari Kubwa