Msigwa akana chadema kuhamasisha vurugu

30Nov 2019
Hellen Mwango
Nipashe
Msigwa akana chadema kuhamasisha vurugu

SHAHIDI wa pili wa utetezi katika kesi ya uchochezi, Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Peter Msigwa, amedai mahakamani kwamba chama chake kilitumia lugha ya picha katika mikutano ya kampeni ili kuhamasisha kukichagua.

Kadhalika, amedai kuwa tuhuma zinazomkabili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, hazina ukweli bali zimetokana na kutoeleweka lugha za kisiasa kati ya Chadema na Jamhuri.

Msigwa alitoa madai hayo jana wakati akitoa ushahidi wa utetezi wake mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, anayeskiliza kesi hiyo.

"Mheshimiwa hakimu, chama changu kilitumia lugha ya picha  katika mikutano yetu ya kampeni  kwa lengo la kuhamasisha watu kukipigia kura katika uchaguzi mdogo wa ubunge katika Jimbo la Kinondoni,” alidai.

"Pia mwenyekiti wetu  alihamasisha watu kupiga kura ili kuongeza nguvu katika kambi ya upinzani, kuongoza mapambamo ni kuonyesha wananchi masuala  yanayokiukwa na kuyadai kwa mujibu wa katiba," aliongeza.

Mapema upande wa Jamhuri ukiongozwa na Mkurugenzi wa Mashtaka Msaidizi, Faraja Nchimbi, ulimhoji mshtakiwa wa kwanza, Mwenyekiti Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe, dhidi ya utetezi wake.

Mbowe alidai kuwa  hajui kama kuna ibara yoyote ya katiba au sheria ya nchi inayoelekeza chama cha siasa au mtu kuchukua nchi kwa kumwaga damu, kubeba majeneza, mapanga, marungu au maandamano.

Alidai kuwa tangu awe mbunge kwa miaka 15 sasa, anailinda na kutetea katiba ya nchi miongoni mwa viapo wanavyokula wakati wa kuapishwa na kwamba ana ufahamu wa baadhi ya sheria za nchi.

Alidai moja ya majukumu yake kama mbunge ni kutunga sheria za nchi, kufanya marekebisho ya sheria na aliwahi kushiriki na kwamba nchini utaratibu wa kubadilishana uongozi ni wa mihula.

Mbowe aliendelea kudai kuwa si sera ya chama chake kuhamasisha chuki, kutembea na silaha hadharani au kuhamasisha chuki katika jamii na kuvunja sheria za nchi.

Alidai hakumbuki katika ushahidi wake aliwahi kusema kama kuna mtu alikufa kwa kupigwa na risasi katika mfululizo wa mkutano wa kufunga kampeni uliofànyika katika viwanja vya Buibui Mwananyamala hadi eneo la Mkwajuni.

Mbiwe alidai Kwamba mkutano huo ulifanyika Februari 16, mwaka jana na kwamba hakushiriki kukagua watu walioudhuria mkutano huo kujua kama walikuwa na silaha au la.

Mbali na Mbowe na Msigwa, washtakiwa wengine ni Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu;  Mbunge wa Kibamba, John Mnyika;  Katibu Mkuu, Vincent Mashinji; na Mbunge wa Bunda, Ester Bulaya.

Wengine ni Mbunge wa Kawe.  Halima Mdee; Mbunge Tarime Vijijini, John Heche, na Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko.

Washitakiwa wanakabiliwa na mashitaka 13 likiwemo la kula njama kwa madai kwamba Februari 1 na 16, mwaka jana, Dar es Salaam walikuĺa njama ya kutenda kosa la kufanya mkusanyiko usio halali na kukiuka tamko kutawanyika.

Pia wanadaiwa kuwa Februari 16, katika barabara ya Kawawa Kinondoni Mkwajuni washtakiwa hao wakiwa na wenzao ambao hawapo mahakamani, walikiuka tamko la kuwataka kutawanyika la ofisa wa polisi, Mrakibu Mwandamizi Gerald Ngiichi kwa kugoma kutawanyika na kupelekea uvunjifu wa amani. 

Inadaiwa kugoma huko kulisababaisha hofu na hatimaye kusababisha kifo cha Akwilina Akwiline na majeruhi kwa askari wawili ambao ni  Konstebo Fikiri na Koplo Rahim Msangi. 

Habari Kubwa