Vifurushi vipya NHIF kaa la moto

30Nov 2019
Elizaberth Zaya
Dar es Salaam
Nipashe
Vifurushi vipya NHIF kaa la moto

CHAMA cha ACT-Wazalendo kimepinga vifurushi vipya vya bima ya afya vilivyotolewa na Mfuko wa Taifa wa Bima (NHIF), kikidai ni mwendelezo wa kuwaumiza wananchi wanyonge.

Katibu Mkuu wa chama cha ACT-Wazalendo, Dorothy Semu

Kauli hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dorothy Semu, alipozungumza na waandishi wa habari.

Vifurushi hivyo vilizinduliwa juzi jijini Dar es Salaam na uongozi wa NHIF, ukieleza kuwa vimegawanywa katika makundi matatu yaliyopewa majina ya 'Ninajali Afya', 'Wekeza Afya' na 'Timiza Afya'.

“Mfumo wa sasa wa bima ya afya unawalenga hasa wananchi walioajiriwa katika sekta za umma na binafsi. Ni  asilimia tisa tu ya Watanzania wenye vigezo vya kuingia katika mfumo wa bima.

"Na mpaka sasa, (mfuko) unahudumia wanachama 966,792 sawa na wanufaika 4,025,693 kwa mujibu wa taarifa za Mkurugenzi wa mfuko huo.

“Kwa hiyo, asilimia 91 ya nguvu za Watanzania haimo kwenye bima ya afya. NHIF imetangaza vifurushi vipya kwa maelezo kuwa itafikia watu wengi zaidi.

"Hii ni hadaa kwa wananchi. Serikali imeamua kujiweka kando kwenye wajibu wa kutoa huduma za afya kwa watu wengi hasa maskini.

“Takwimu za Hali ya Uchumi wa Taifa, zinaonyesha kuwa mwaka 2018, Watanzania milioni 41 walikuwa wagonjwa wa nje kwenye hospitali, vituo vya afya na zahanati nchi nzima.

"Hii ina maana kuwa asilimia 77 ya Watanzania waliumwa mwaka 2018, likiwa ni ongezeko la asilimia 17 la walioumwa mwaka 2017. Katika nchi ambayo raia wake wanaumwa kwa kiwango hiki, suala la afya linapaswa kuchukuliwa kwa uzito mkubwa sana," alisema.

Semu aliongeza kuwa kitendo cha serikali kujiondoa kwenye kuhudumia raia wake kwenye afya kwa kutangaza vifurushi vipya vya bima, ni kuwatenga wenye kipato cha chini.Alisema gharama zilizowekwa katika vifurushi hivyo vipya zinajenga matabaka mawili katika utolewaji wa huduma za afya; la wenye nacho na wasio nacho.

“Binadamu hachagui kuumwa au aina ya ugonjwa ambao unapaswa kuugua, utaratibu huu wa vifurushi unachukulia kwamba suala la ugonjwa ni jambo la hiari, kwamba mtu anaweza kuchagua kuumwa ugonjwa huu ama kuukataa ule, hivyo atatibiwa kutokana na chaguo lake.

"Mtazamo wa namna hii ni hatari sana katika ujenzi wa jamii yenye utu, usawa na yenye haki. Duniani kote kuna bima aina mbili, ya binafsi na ya umma. Kiwango cha malipo ya kila mwaka kwa kila mtu ni tofauti kulingana na vigezo tofauti.

"NHIF kimsingi ni skimu ya bima ya afya ya umma, na kwa maana hiyo viwango vya malipo vinatokana na uwiano wa kipato cha mtu na mafao yanapaswa kuwa sawa kwa watu wote bila kujali kiasi cha mchango wanaotoa.

"Kitendo cha kutoa vifurushi vya malipo tofauti, na huduma kutolewa kwa kuzingatia kifurushi, ni kitendo cha kuifanya NHIF kuwa bima binafsi na 'kubidhaisha' afya ya Watanzania," alidai.

Chama hicho kilishauri kusimamishwa kwa huduma ya vifurushi hivyo vipya ili kupunguza matumizi makubwa ya rasilimali fedha.

“Kwa mfano, badala ya kuzuia wananchi wa kipato cha chini kupata huduma mbalimbali kama MRI na CT scan, serikali itoe ruzuku kwa wananchi hao kwa kuwalipia NHIF. Huu ndiyo wajibu wa serikali kutokana na kodi inazokusanya kutoka kwa wananchi,” alisema.

Chama hicho pia kilitoa wito kutazamwa upya mfumo wa hifadhi ya jamii ili ndani yake kuwe na bima ya afya kwa Watanzania wote na kwamba kwa kutumia utaratibu huo, hifadhi ya jamii itasaidia wananchi kujiwekea akiba.

Habari Kubwa