Asimulia alivyofukuzwa kazi kwa kukataa rushwa ya ngono

02Dec 2019
Elizaberth Zaya
Nipashe
Asimulia alivyofukuzwa kazi kwa kukataa rushwa ya ngono

MADHARA yanayowapata baadhi ya wafanyakazi wanawake kazini kwa kuombwa rushwa ya ngono ni pamoja na kunyanyasika au kufukuzwa kazi wanapokataa kutimiza matakwa ya mabosi wao.

Stell Igidio, ni mmoja wa wafanyakazi aliyepitia changamoto hiyo na anasimulia namna alivyofukuzwa kazi baada ya kukataa kushiriki ngono na bosi wake na kukutana na 'vigingi' vya kuombwa rushwa ya ngono akitafuta haki yake ya kurudishwa kazini.

Akihojiwa katika moja ya televisheni zinazoendesha shughuli zake kwa njia ya mtandao, Stella ambaye alitafuta haki yake na kurudishwa kazini baada ya kushinda kesi, alisema alifukuzwa kazi kwa kukataa kusafiri na mkuu wake wa kazi aliyemwomba asafiri naye kwa ajili ya mapumziko ya kimapenzi.

"Bosi wangu aliniita siku moja akaniambia kwamba anataka asafiri na mimi ‘weekend’ kwenda nje ya mkoa kwenye mapumziko ya kimapenzi na pia kwenda kuitangaza taasisi yake huko, nilishtuka sana na sikukubaliana na suala hilo," alisema Stella.

"Baada ya kukataa, akabadilisha na kusema basi twende weekend iliyokuwa inafuata, pia nikakataa kwa kumwambia nashukuru kwa ofa lakini sitakwenda."

Kitendo cha kukataa mara kadhaa ombi la mkuu wake wa kazi, alisema kilisababisha aanze kufanyiwa visa hadi kufukuzwa kazi.

Hata hivyo, Stella alisema hakukubaliana na hatua ya kufukuzwa kazi kwa kuamini kuwa hakuwa na kosa.

"Niliomba ushauri kwa wanasheria baada ya kufukuzwa ili kufahamu namna ya kupata haki yangu na waliniambia kwamba nianze kwa kukata rufani katika bodi ya kazini kwangu, nilifanya hivyo kwa kumtafuta mwenyekiti wake ambaye naye alinikatisha tamaa baada ya kuniambia ili nishinde natakiwa kuwa karibu naye sana," alisema Stella.

"Alikuwa anataka niwe naye kimapenzi na akinihakikishia kwamba nikikubali kufanya hivyo nitashinda na nitarejeshwa kazini, nilikataa kabisaa na ndipo baada ya siku chache nikapewa barua kwamba rufani yangu imetupiliwa mbali.”

Pamoja na kikwazo hicho, Stella alisema hakukata tamaa na kuamua kwenda kushtaki katika vyombo mbalimbali ambavyo alikutana na hali hiyo ya kuombwa rushwa.

"Baada ya miaka miwili niliposhindwa kupata haki kote nilikozunguka, ilibidi niende Tume ya Usuluhishi na Maamuzi ambako nashukuru Mungu nilishinda na iliamua nilipwe mishahara ya miezi 12," alisema Stella.

"Nilipotafakari niliona kwamba uamuzi ule haukunisaidia sana kwa sababu haukusema nirudishwe kazini isipokuwa nilipwe mshahara wa miezi 12 tu wakati mpaka uamuzi huo unatolewa tayari nilikuwa nimekaa zaidi ya miaka mitatu nje ya kazi. Sikuridhika, libidi niende Mahakama Kuu divisheni ya kazi."

"Hivi ninavyozungumza mwaka jana mwezi wa nane nilishinda kesi, nililipwa haki zangu zote katika kipindi chote ambacho nilifukuzwa na nimerudishwa kazini."

"Nataka niwaambie wote wanaosumbuliwa na jambo hili kazini, wasikubali kutoa rushwa ya ngono kwa ajili ya kupata jambo fulani au kunyanyaswa, wajenge tabia ya kukimbilia kwenye vyombo vya sheria maana inawezekana kupata haki bila kutoa rushwa.

Hivi karibuni katika Maadhimisho ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia, Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP- Mtandao, Lilian Liundi, alisema takwimu zilizotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) mwaka 2015/2016 zinaonyesha kuwa vitendo vya ukatili wa kingono vinaongezeka kulingana na umri.

Liundi alisema ripoti ya idadi ya watu duniani ya mwaka 2019 inaonyesha kuwa asilimia 35 ya wanawake wote duniani wamekutana na aina mbalimbali za ukatili ikiwamo udhalilishaji wa kingono katika maisha yao.

Habari Kubwa