Ronaldo kundi gumu Euro 2020

02Dec 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Ronaldo kundi gumu Euro 2020

MABINGWA wa Ulaya, Timu ya Taifa ya Ureno wamepangwa katika Kundi F pamoja na vigogo, washindi wa Kombe la Dunia, Ujerumani na Ufaransa katika mashindano ya kuwania ubingwa wa Kombe la Euro 2020.

Ratiba hiyo iliyotolewa usiku wa kuamkia jana inaonyesha kuwa, Ujerumani itacheza mechi ya ufunguzi dhidi ya Ufaransa katika mashindano hayo yanayotarajiwa kufanyika kuanzia Juni 12 hadi Julai 12, mwakani.

Katika kinyang'anyiro hicho, Kundi A linaundwa na Italia, Uswisi, Uturuki na Wales wakati Ubelgiji, Urusi, Denmark, Finland wanaunda Kundi B huku Ukraine, Uholanzi, Austria na timu nyingine, zimepangwa kwenye Kundi C.

England, Croatia, Jamhuri ya Czech na nyingine itakayojulikana baadaye kati ya Scotland, Israel, Norway au Serbia zenyewe ziko katika Kundi D.

England yenye itaanza kampeni zake kwa kuwavaa Croatia, mchezo utakaochezwa kwenye Uwanja wa Wembley, huku kwa mara nyingine tena ikipangwa dhidi ya timu ya Jamhuri ya Czech.

Kikosi hicho kinachonolewa na Gareth Southgate, mwaka jana kilitolewa na Croatia katika hatua ya nusu fainali ya mashindano ya Kombe la Dunia.

Mashindano hayo yamepangwa kuchezwa katika mataifa 12 za Ulaya, mfumo ambao umewekwa maalumu kusherehekea miaka 60 ya kuanzishwa kwa michuano hiyo ya Ulaya.

Habari Kubwa