Timuatimua makocha Simba, Yanga chanzo kuvurunda Caf

02Dec 2019
Mhariri
Nipashe
Timuatimua makocha Simba, Yanga chanzo kuvurunda Caf

HATIMAYE baada ya tetesi zilizodumu kwa takribani wiki mbili kuhusu kutimuliwa kwa Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Aussems, zimetimia mwishoni mwa wiki, kufuatia uongozi wa klabu hiyo kutangaza kuvunja mkataba rasmi na Mbelgiji huyo.

Simba, mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, imesitisha mkataba wa kocha huyo ikiwa ni wiki tatu hivi tangu watani zao wa jadi, Yanga walipomtimua Kocha Mkuu, Mkongomani Mwinyi Zahera.

Kocha huyo wa Yanga, alitimuliwa kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kutokana na kushindwa kuiunganisha timu hiyo kucheza vizuri jambo lililosababisha kutolewa kwenye michuano ya kimataifa na Pyramids FC ya Misri kwa jumla ya mabao 5-1.

Aidha, uongozi wa Yanga ulifafanua kuwa haukuona sababu kwa Zahera kushindwa kufanya vizuri kwa kuwa idadi kubwa ya wachezaji katika kikosi chake walisajliwa kutokana na mapendekezo yake.

Zahera aliyerithi mikoba ya Mzambia George Lwandamina msimu uliopita akatimuliwa wakati timu hiyo ikiwa imecheza mechi tatu ikipoteza moja, sare moja na kushinda mchezo mmoja, hivyo timu kukabidhiwa kwa Kaimu Kocha Mkuu, Boniface Mkwasa.

Kwa upande wa Aussems aliyerithi mikoba hiyo kutoka Mfaransa Pierre Lechantre Julai mwaka jana, ametimuliwa wakati timu hiyo ikiwa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu, imejikusanyia pointi 25 baada ya kucheza mechi 10, ikishinda nane, sare moja na kupoteza mchezo mmoja.

Hata hivyo, Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mazingisa, katika taarifa yake ameeleza kuwa uongozi umefikia hatua hiyo ya kumtimua Aussems kutokana na kushindwa kufikia malengo na viwango walivyokubaliana na klabu.

Katika taarifa yake imeeleza zaidi kuwa pamoja na Aussems kupewa ushirikiano hata baada ya kutolewa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo malengo ilikuwa kufika hatua ya makundi ameendelea kusimamia bila kujali malengo ya Simba.

Malengo akiyataja kuwa ni kujenga timu yenye ari na mafanikio, nidhamu na ushindani kwenye mashindano ya ndani na nje ya nchi.

Kwa ujumla hatuwezi kupinga uamuzi uliofikiwa na Simba kama ambavyo pia tulishaeleza wakati Yanga ilipomtimua Zahera, kwa kuwa makocha hao wameshindwa kufikia malengo ya waajiri wao kama kweli yalikuwapo katika mikataba yao.

Lakini kinachotusikitisha na kutufanya kuamini itazichukua muda mrefu klabu hizi mbili kuweza kufikia malengo yao kwenye michuano ya kimataifa, ni kutokana na tabia ya timuatimua hii ambapo makocha huwa hawamalizi zaidi ya msimu mmoja.

Tulitarajia kama ambavyo inaelezwa Zahera alipewa nafasi ya kupendekeza wachezaji wakusajiliwa na hata Aussems ambaye inadaiwa alitoa mapendekezo lakini hayakuzingatiwa kama alivyohitaji, wangedumu na klabu hizo kwa angalau misimu miwili ama mitatu.

Tunatambua ili kuweza kufanya vizuri katika michuano ya kimataifa, Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika ni pamoja na kocha kupata muda wa kutosha kuzifahamu mbinu, ugumu na hata fitina zilizopo kwenye mashindano hayo.

Lakini sasa, muda si mrefu klabu hizo zitatangaza makocha wapya na wanaweza wasiwe wameshawahi kuziongoza timu kwenye michuano hiyo Caf, lakini huenda wasipate hata nafasi ya kufanya usajili wanaoutaka.

Hivyo, ni wazi wakiingia katika michuano hiyo watakuwa wanaanza upya, huku wakihitaji muda zaidi kuvisuka vikosi vyao, jambo litakalozifanya kila msimu kuwa wasindikizaji.

Habari Kubwa