Kipa Zanzibar Queens asilie, atakuwa imara

02Dec 2019
Adam Fungamwango
Nipashe
Kipa Zanzibar Queens asilie, atakuwa imara

TUKIO la golikipa wa Timu ya Soka ya Wanawake ya Zanzibar Queens, Hajra Abdallah, kuangua kilio baada ya kufungwa mabao 7-0 dhidi ya Tanzania Bara katika mechi ya mashindano ya Kombe la Chalenji, yaliyomalizika hivi karibuni, lilisikitisha wengi waliokuwa wakiangalia pambano hilo.

Ilikuwa ni mechi ya Kundi B ya michuano hiyo iliyoanza Novemba 16 hadi 25, mwaka huu kwenye Uwanja wa Azam Complex, jijini Dar es Salaam na kikosi cha Kenya kutwaa ubingwa, uliokuwa unashikiliwa na wenyeji, Kilimanjaro Queens ya Tanzania Bara.

Kabla ya hapo Zanzibar ilikuwa imeshapoteza mechi mbili, dhidi ya Burundi na Sudan Kusini ambazo zote walikula mabao 5-0 kila mechi.

Wakati wenzake wameshikana mikono na ndugu zao wa Bara wakizunguka kuonyesha ishara ya upendo kwa kuwa wote ni ndugu moja, Hajra yeye alikuwa akibembelezwa na baadhi ya watu waliokuwa kwenye benchi ya ufundi la timu yake.

Golikipa huyo alilia kwa uchungu na kwa hisia kubwa. Wengine wanasema alikuwa analia kwa sababu aliona kama amewafungisha wenzake. Baadhi wanasema huenda wenzake walimlaumu kwa kufungwa magoli mepesi ndiyo maana amechukia na kulia.

Ukweli ni kwamba Hajra alikuwa akilia kwa sababu ni mshindani wa kweli. Kufungwa kwake ilikuwa ni kitu kilichomuumiza sana. Kwa nini afungwe? Alikuwa pia na uzalendo na Zanzibar.

Mchezaji mzuri mara nyingi ni yule ambayo anachukia kupoteza mechi.

Tatizo lilikuwa moja tu, uwezo. Hakuwa na uwezo wa kuzuia mashuti makali ya yaliyopigwa na Asha Rashid, Philomena Kizima, Donesia Minja na wengineo.

Si kwa sababu hana uwezo wa kukaa golini na kudaka, la hasha. Kwanza kabisa matatizo yanaanzia kwenye maandalizi ya timu yenyewe ya Zanzibar ambayo yalikuwa ya zimamoto, nadhani na pia kiuchumi haikuwa sawa.

Pili ni kwamba ukimwangalia Hajra ni mmoja wa wachezaji mwenye umri mdogo kwenye michuano hiyo.

Ukitafuta wachezaji watano kwenye michuano hiyo wenye umri mdogo, miongoni mwao atakuwa ni kipa huyo wa Zanzibar aliyedaka mechi hiyo dhidi ya Tanzania Bara.

Kwa maana hiyo umbile lake la kitoto, ndilo kwa kiasi kikubwa lilimfanya afungwe magoli yale.

Pamoja na kufungwa magoli yote hayo, lakini bado kuna wakati Hajra alikuwa akidaka mipira vizuri, kupangua, kupanga mabeki vizuri kwenye faulo na kuwafokea pale wanapojisahau, tofauti na umri wake pamoja na wenzake.

Kitu kingine kwa Hajra ni kwamba anaonekana anapenda kucheza. Anaupenda mchezo wenyewe na anafurahia kucheza.

Benchi la ufundi la Zanzibar Queens bado lina nafasi ya kumwendeleza kwa kumtunza golikipa huyo kwani inaonekana baadaye atakuja kuwa kipa nzuri sana si kwa Zanzibar, bali hata Tanzania yote.

Kitu kizuri kwa Hajra ni kwamba ameuanza mchezo wa soka akiwa na umri mdogo, hivyo baadaye atakuwa na kukomaa akiwa ndani ya soka.

Mara nyingi wacheza soka wanawake huanza mchezo huo wakiwa wakubwa, na hata kuna taarifa kuwa baadhi ya wachezaji wa Zanzibar walichukuliwa kutoka kwenye mchezo wa netiboli na kuletwa kucheza soka.

Yale mashuti aliyokuwa anapigiwa na kina Mwanahamisi Omari kila anapozidi kukua na kucheza soka atayazoea. Baada ya miaka miwili na kuendelea atakuwa mrefu, hivyo hatokuwa na matatizo tena na mipira ya juu.

Ukichanganya na kujituma kwake na kuupenda mchezo wa soka, atapata uzoefu na mafunzo na kuwa kipa mzuri na tegemeo kwa taifa.

Ana uwezo mzuri wa kuruka na hata 'timing', ila makocha itabidi wampe zaidi mazoezi ya mikono ili aweze kudaka bila kutema.

Hajra atakuwa kipa mzuri sana baada ya miaka michache kama ataendelea kucheza soka.

Habari Kubwa