Ubora wa elimu ya awali utaondoa mbumbumbu

03Dec 2019
Sabato Kasika
Nipashe
Ubora wa elimu ya awali utaondoa mbumbumbu

ELIMU ya awali ni nguzo muhimu katika kumjengea mtoto uwezo wa kusoma, kuandika na kuhesabu (KKK) ili wanapoingia darasa la kwanza awe tayari ameandaliwa kikamilifu, katika maeneo hayo matatu muhimu.

Kutokana na umuhimu huo, serikali inahimiza kila shule ya msingi iwe na darasa la elimu ya awali au shule shikizi, ambazo majengo yake yanajengwa kwa nguvu za wananchi.

Miongoni mwa maeneo ambayo kasi ya ujenzi wa shule hizo imepamba moto ni kwenye vijiji mbalimbali vya Musoma mkoani Mara, ambako wananchi wanajitolea kwa hali na mali ili kufanikisha ujenzi huo.

Wanafanya hivyo kuitikia maelekezo ya serikali ya kuhakikisha kila shule ya msingi inakuwa na darasa la shule ya awali kwa ajili ya kuwanoa watoto wanaojiandaa kuingia darasa la kwanza.

Musoma Vijijini ina vijiji 68 na karibu vijiji vyote wananchi wanaendelea na ujenzi wa majengo ya shule shikizi, hatua ambayo itawezesha watoto wote kupata elimu ya awali.

Ujenzi huo unaendelea kila kijiji, kutokana na ukweli kwamba elimu ya awali ni msingi muhimu, kwani elimu ya baadaye inategemea kwa kiasi kikubwa mafanikio ya elimu hiyo.

Kuwapo kwa madarasa hayo ni fursa kwa watoto wote wakiwamo wanaotoka familia duni zisizo za uwezo wa kupeleka watoto katika shule za awali za kulipia, hivyo ni muhimu kuunga mkono ujenzi huo."Tunataka kuhakikisha kila kijiji kinakuwa na shule shikizi, ndiyo maana tunahamasisha wananchi wetu kushiriki kwa hali na mali, katika ujenzi wa shule hizi muhimu," Prof. Sospeter Muhongo anasema.

Profesa Muhongo ni Mbunge wa Musoma Vijijini, anasema wananchi wake wameitikia maelekezo ya serikali, kwa kutambua kuwa elimu ndiyo kila kitu, hivyo hawana budi kuhakikisha wanakuwa na shule shikizi.

Kimsingi ni kwamba nyumba imara inahitaji msingi uliokamilika, hii ikihusisha mahitaji yote muhimu kuanzia msingi bora na imara uliojengwa na fundi mwenye weledi wa hali ya juu, akizingatia ubora vifaa anavyotumia.

Iwapo hilo halitafuatwa katika kujenga msingi imara, nyumba itaanguka wakati wowote na inawezekana ikaanguka wakati ujenzi ukiendelea au miaka michache baada ya ujenzi kukamilika. 

Hivyo ndivyo ilivyo hasa kwenye elimu, kwamba elimu ya awali iliyo bora ndiyo msingi wa kupata wahitimu walio bora katika ngazi zote za kitaaluma. Umuhimu wake hauwezi kulinganishwa na kitu chochote kile.

Kwa ujumla ni kwamba, elimu ya awali ndiyo inayomwandaa na kujenga msingi mzuri kwa mtoto kabla ya kuanza darasa la kwanza, sekondari na hatimaye kuhitimu masomo ya chuo kikuu.

Hivyo ili kuhakikisha kuwa elimu ya awali inatolewa kwa watoto wote,  serikali iliagiza, katika kila shule ya msingi lazima ianzishwe darasa la elimu ya awali, ili kuwaandaa wanafunzi kuingia darasa la kwanza.

Serikali ilifikia uamuzi huo kupitia Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 1995 na tamko la Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi la mwaka 2010, na sasa ujenzi wa madarasa hayo umekamilika na mengine yakiendelea.

Iwapo nchi nzima itakuwa na madarasa hayo, huku elimu ya awali ikitolewa katika misingi inayotakiwa, itakuwa ni njia bora na nzuri ya kuimarisha ubora wa elimu kuanzia awali hadi ngazi ya juu.Hatua hii ikiimarishwa inaweza kumwondoa adui ujinga ambaye anasababisha kuwapo kwa watu wasiojua kusoma na kuandika, kuanzia kwa vijana hadi watu wazima.

Ni muhimu Watanzania kuunga mkono hatua hii inayolenga kuboresha elimu ya awali kabla ya kupanda ngazi nyingine za juu, kwani ndiko ambako mtoto anatakiwa kutoka akiwa anajua kusoma, kuandika na kuhesabu.

Kuwapo kwa shule hizo kutasaidia kumaliza tatizo la kuwapo kwa Watanzania wasiojua kusoma, kuandika na kuhesabu, kwa sababu watakuwa wamepata msingi mzuri wa elimu kuanzia shule za awali.Sera mpya ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 iliyozinduliwa na Rais mstaafu Jakaya Kikwete mwaka 2015, suala la elimu ya awali limepewa kipaumbele.

Habari Kubwa