Vijana wajitambue, wachukue tahadhari maambukizi ya VVU

03Dec 2019
Mhariri
Nipashe
Vijana wajitambue, wachukue tahadhari maambukizi ya VVU

Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani kwa mwaka huu, yameacha ujumbe mzito kwa vijana weti nchini, kwamba wanakabiliwa na hatari kubwa ya kuambukizwa Virusi vya Ukimwi (VVU).

Kwa kijana makini anayejitambua na thamani ya maisha yake binafsi na kwa taifa, bila shaka akisoma takwimu zilizotolewa wakati wa maadhimisho ya mwaka huu jijini Mwanza Jumapili, atatanya tafakuri na kujitathmini kuhusu maisha yake.

Kimsingi, kundi vijana hasa wa kike linadaiwa kuongoza kwa kuwa na maambukizi mapya ya VVU kwa mujibu wa takwimu za maambukizi ya virusi hivyo kwa mwaka 2016/2017.

Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani yaliyofanyika katika Uwanja wa Rock City Mall jijini Mwanza, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, alisema katika maambukizi mapya 72,000 vijana ni asilimia 40 na kati ya hao asilimia 80 ni wa kike.

Takwimu hizi zinadhihirisha kuwa kundi la vijana hasa wa kike ndilo linaloonekana kuwa kwenye hatari kubwa ya kupata maambukizi mapya ya VVU.

Waziri Mhagama alisema miongoni mwa sababu ni pamoja na ngono zembe katika umri mdogo, hali inayosababisha mhusika kuwa na wapenzi wengi, inayojenga hatari ya kupata maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi.

Alisema serikali kwa kushirikiana na wadau wamejitoa kuelimisha umma hasa kwenye mikusanyiko ili kupunguza maambukizi mapya katika jamii.

Aliwasihi watu wanaoishi na virusi hivyo kuendelea kutumia dawa na wanaume kuacha kuwarubuni vijana wadogo kwa lengo la kufanya nao mapenzi.

Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, alisema wameshusha umri wa vijana kupima maambukizi ya VVU bila kupata ridhaa ya mzazi au mlezi kutoka miaka 18 hadi miaka 15 na kuwasihi vijana kupima afya zao ili wapate kufahamu na watakaobainika kuwa na maambukizi kuanza dawa mapema.

Tunaunga mkono jitihada zinazofanywa na serikali katika kupunguza kama siyo kutokomeza maambukizi ya VVU ikiwamo kutoa elimu kwa umma.

Hata hivyo, takwimu zilizotolewa Jumapili zinatufanya tuwaone vijana kuwa sasa nduo wananyemelewa na hatari ya VVU na Ukimwi. Hivyo tunawashauri kushtushwa ba takwimu hizo na kuchukua hatua ya kujilinda dhidi ya kasi hii kubwa ya maambukizi.

Tahadhari iwe kujitambua kuwa wao ndio nguvu kazi ya familia na taifa kwa ujumla hususan kutojiingiza kwenye ulevi, dawa za kulevya pamoja na kufanya ngono zembe.

Takwimu hizi mpya pia zinaonyesha jinsi wasichana walivyo katika hatari zaidi ya kuambukizwa VVU na Ukimwi kwa kuwa zinaeleza kuwa asilimia 80 ya vijana wanaoambukizwa ni wasichana.

Hii ina maana kubwa, kaasi cha kutufanya Nipashe kuitafsiri halii hii kuwa wasichana wengi ni wepesi wa kurubuniwa na wanaume na kufanya nao ngono bila tahadhari; kwa maana ya kutotumia kondomu.

Na vilevile, inatushawishi kuamini kuwa wasichama wengi wa umri huo wanajihusisha na na biashara ya ngomo, na wanakosa msimamo wa kuwakatalia wanaume wanapowashawishi au kuwalazimisha kufanya nao ngomo bila kinga.

Ni wakati mwafaka sasa kwa vijana wote kutambua kuwa Ukimwi unaua , na ni ugonjwa ambao hadi sasa hauna kinga wala tiba, na njia pekee ya kuepukana nao ni kuchukua tahadhari. Hivyo hawanabudi kuchukua hatua sasa.

Habari Kubwa