Kichocho, minyoo tishio Mwanza

03Dec 2019
Anthony Gervas
MWANZA
Nipashe
Kichocho, minyoo tishio Mwanza

UGONJWA wa kichocho na minyoo ya tumbo vimetajwa kuwa tisho katika Mkoa wa Mwanza, huku wilaya ya Ukerewe ikiongoza kwa maambukizo.

Hayo yaliyobainishwa na Mratibu wa Magonjwa yasiyopewa Kipaumbele mkoani Mwanza, Dk. Mabai Thobias, katika mahojiano maalum na Nipashe jijini humo mwishoni mwa wiki.

“Takwimu kutoka katika vituo vya kukusanyia taarifa za afya mkoani Mwanza, mwaka 2018 zinaonyesha watu waliokuwa wameathirika na ugonjwa wa kichocho pekee, Wilaya ya Ukerewe watu 1,765, Buchosa 1,000, Nyamagana 600 na Ilemela 572.

“Ugonjwa wa kichocho upo, hakuna wilaya iliyo salama katika Mkoa wa Mwanza, Ilemela na Nyamagana zaidi ya asilimia 80 kuna kichocho na iligundulika katika utafiti wa afya kuwa jamii inayoishi kando ya Ziwa Victoria iko hatarini zaidi. Kati ya watu 10, wanane au saba wanakuwa wameathirika," alibainisha.

Kwa upande wa minyoo, Dk. Thobias alisema: Mkoa wa Mwanza mwaka jana ulikuwa na wagonjwa 17,000, Ilemela ilikuwa na zaidi ya wagonjwa 9,000, Ukerewe zaidi 7,000, Sengerema zaidi ya 5,000 na Buchosa zaidi watu 5,000."

Alisema kwa ujumla, wilaya zote za mkoa huo ambazo ni Ilemela, Nyamagana, Magu, Misungwi, Sengerema, Buchosa na Kwimba watu wake wameathirika na magonjwa ya kichocho na minyoo ya tumbo.

“Kundi linaloathirika zaidi na ugonjwa wa minyoo ya tumbo ni watoto wenye umri wa kwenda shule kuanzia miaka mitano hadi watu wazima miaka 60.

"Tatizo hili linachagizwa na kutumia vyakula visivyokuwa salama, hasa kachumbali, karoti, kabichi na kutonawa mikono watu wanapotoka kujisaidia chooni, kutembea peku na kutokuwa na vyoo," alisema.

Akifafanua zaidi kuhusu kichocho, Dk. Thobias alisema kinasababishwa na vimelea vya Schistosoma ambavyo vinaenezwa na konokono.

Alisema ugonjwa huo uko katika aina mbili ambazo ni kichocho cha tumbo na kichocho cha kibofu cha mkojo.

Alisema maambukizo ya ugonjwa huo kuenezwa na konokono, akibainisha kuwa binadamu anapokwenda kujisaidia haja ndogo au kubwa katika vyanzo mbalimbali vya maji, kama ana ugonjwa huo, huacha mayai yake katika vyanzo hivyo na baadaye hupevuliwa na konokono.

Alisema kuwa baada ya kupevuliwa mayai hayo na husambaa ndani ya maji, hivyo yakitumiwa na binadamu, anapata maambukizo ya ugonjwa huo.

Dk. Thobias alisema dalili za ugonjwa huo ni pamoja na kuumwa tumbo na kukojoa damu na kwamba mgonjwa akichelewa kupata matibabu, huathirika kwa mfumo mzima wa chakula ndani ya tumbo, kupata kansa ya kibofu cha mkojo na hata kupoteza maisha.

Mtaalamu huyo wa afya alisema wavuvi wa Ziwa Victoria ndiyo kundi lililoko katika hatari zaidi ya kuathirika kwa kichocho kutokana na shughuli zao za kukaa kwenye maji kwa muda mrefu.

Dk. Thobias aliwataka wananchi kujenga utamaduni wa kuzingatia kanuni za afya kwa kwenda kupima afya zao mara kwa mara na kuachana na kasumba ya kubuni matibabu wakiwa nyumbani kwa dawa za miti shamba.

Habari Kubwa