Papa Msofe kortini tuhuma uhujumu uchumi

03Dec 2019
Hellen Mwango
Nipashe
Papa Msofe kortini tuhuma uhujumu uchumi

WAFANYABIASHARA wanne akiwamo Marijan Msofe (53), maarufu kama ‘Papa Msofe’ na Wakili wa Kujitegemea, Mwesigwa Mhingo (36), wamefikishwa mahakamani wakikabiliwa kesi ya uhujumu uchumi ikiwamo kuratibu genge la uhalifu na kutakatisha Dola za Marekani 410,000 (sawa na Sh. milioni 943).

Mbali na Papa Msofe na Mhingo, washtakiwa wengine ni Wenceslaus Mtui (49), Josephine Haule (38) na Fadhili Mganga (61).

Washtakiwa hao walisomewa mashtaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Huruma Shaidi anayesikiliza kesi hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.

Upande wa Jamhuri uliongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu Maternus Marandu, Wakili wa Serikali Mwandamizi Ladislaus Komanya na Wakili wa Serikali Glory Mwenda.

Komanya alidai kuwa katika tarehe tofauti kati ya Desemba 2018 na Septemba, mwaka huu, washtakiwa wote kwa pamoja na wenzao ambao hawajakamatwa walifanya mpango wa kuongoza genge la uhalifu.

Katika shtaka la pili, ilidaiwa kuwa kati ya Desemba, mwaka jana na Septemba, mwaka huu, washtakiwa wote, mahali tofauti, walitakatisha Dola za Marekani 300,000 (sawa na Sh.milioni 690) kutoka kwa Pascal Jean Camille.

Shtaka la tatu,  ilidaiwa kuwa siku ya tukio la pili, washtakiwa wakiwa na nia ovu,  walijipatia kwa njia ya udanganyifu Dola za Marekani 300,000 kutoka kwa Camille baada ya kumdanganya kuwa wangemuuzia kilo 200 za madini aina ya dhahabu na kuyasafirisha kwenda Ureno huku wakijua si kweli.

Upande wa Jamhuri ulidai katika shtaka la nne, katika tarehe tofauti kati ya Desemba mwaka jana na Septemba, mwaka huu washtakiwa walitakatisha Dola za Marekani 110,000 (Sawa na Sh.milioni 253) kutoka kwa John Mahsson wakati wakijua ni zao la uhalifu.

Komanya alidai katika shtaka la tano, washtakiwa walijipatia Dola za Marekani 110,000 kutoka kwa Mahsson baada ya kumlaghai kwamba wangemuuzia kilo 20 za madini aina ya dhahabu na kusafirisha mpaka Ureno huku wakijua si kweli.

Washtakiwa hawakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.

Upande huo wa Jamhuri ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika, hivyo kuomba tarehe nyingine ya kutajwa.

Hakimu Shaidi alisema kesi hiyo itatajwa tena Desemba 16, mwaka huu, na washtakiwa wapelekwe mahabusu.

Habari Kubwa