Vyuo vya fedha vyatakiwa viwango kimataifa

03Dec 2019
Mary Geofrey
Nipashe
Vyuo vya fedha vyatakiwa viwango kimataifa

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, amevitaka vyuo vya fedha nchini kutoa elimu inayoendana na viwango vya kimataifa ili kukidhi mahitaji ya soko la dunia na ukuaji wa uchumi.

Dk. Mpango aliyasema hayo mwishoni mwa wiki katika mahafali ya 45 ya Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), ambayo mgeni rasmi alikuwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Alisema chuo cha IFM ni cha mfano katika kufikia malengo hayo na kwamba serikali inaendelea kukifadhili chuo hicho ili kuzalisha watalaam wenye vigezo vya kufikia malengo ya nchi katika kukuza uchumi wa taifa.

"Hivyo naendelea kusisitiza tena, jukumu la chuo hiki ni kutoa wahitimu wenye weledi na ujuzi wa hali ya juu. Lakini wawe wazalendo kweli kwa nchi yetu, wanaochukia rushwa, ufisadi na waliodhamiria kutoa mchango mkubwa kwa nchi yetu," alisema Mpango.

Dk. Mpango alisema serikali inatambua umuhimu wa chuo hicho na kwamba itaendelea kukijengea uwezo, kuboresha mioundombinu na kuongeza rasilimali watu ili kuendelea kutekeleza malengo yake kwa ufanisi.

Alisema katika nchi zilizoendelea kwa kasi walikuwa na mifumo madhubuti ya usimamizi wa fedha katika serikali, taasisi za umma, benki na bima hivyo Tanzania inatakiwa kuiga mfano.

Aliahidi kuwa serikali itaendelea kulipa mishahara ya watumishi wa chuo hicho ambayo ni Sh. bilioni 11 ambazo Hazina wanazilipa kila mwaka.

Naye Kaimu Mkuu wa chuo hicho, Dk. Immanuel Mvaza, alisema ili serikali iweze kufikia lengo la kukuza uchumi wa viwanda ifikapo 2020, wanahitajika watalaam wa kutosha wa biashara za kimataifa kutoka chuo hicho.

Alisema kwa miaka 19 wanashirikiana na Chuo Kikuu cha Biashara za Kimataifa cha India (IIFT), kwa ajili ya kuzalisha wataalam wa usimamizi wa biashara za kimataifa ambao watawezesha kufikia lengo hilo la kukuza uchumi.

Habari Kubwa