‘Udhibiti Ukimwi usitegemee wahisani wa nje’

03Dec 2019
Na Mwandishi Wetu
MWANZA
Nipashe
‘Udhibiti Ukimwi usitegemee wahisani wa nje’

SERIKALI imetakiwa kuhamasisha kampuni kubwa nchini kuchangia Mfuko wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi ili kuepuka utegemezi kwa wahisani nje ya nchi.

Meneja wa Mgodi wa Geita Gold Mine (GGM), kitengo cha afya, usalama na mazingira, Dk. Kiva Mvungi, alisema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani yaliyofanyika jijini Mwanza.

Dk. Mvungi alisema ili kufanikisha mapambano dhidi ya virusi vya Ukimwi lazima kuwapo na juhudi na nia kwa wanasiasa ya kuongeza mapato katika mfuko huo.

"Ni vyema serikali ihamasishe kampuni kubwa kama za simu, usafirishaji, uzalishaji na mengine,” alisema.

Dk. Mvungi alisema mgodi huo wenye wafanyakazi karibu 5,000 una sera na miongozo mbalimbali kwa wafanyakazi ikiwamo kutoa elimu, kupima afya bure na kutoa huduma ya matibabu kwa wenye maambukizi ya virusi vya Ukimwi.

Mgodi huo unatoa Sh. milioni 750 kila mwaka ukishirikiana na Tume ya Kudhibiti Ukimwi nchini (Tacaids) kwa ajili ya kupambana na Ukimwi na Sh. milioni 250 kati ya hizo zinaingizwa katika Mfuko wa Taifa wa Ukimwi.

Mkurugenzi wa Tacaids, Dk. Leonard Maboko, alisema mchango wa wadau ni muhimu kuwezesha mapambano hayo na uzinduzi wa maadhimisho hayo ulianza kwa matembezi ya hisani yaliyoongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella na kupatikana Sh. 570,000.

Akitoa tathmini ya upimaji uliofanyika tangu kuanza kwa maadhimisho hayo, Novemba 25, mwaka huu hadi siku ya kilele Desemba Mosi, Dk. Maboko alisema watu 2,265 walipima virusi vya Ukimwi.

Dk. Maboko alizishukuru taasisi zote, vyombo vya habari na kampuni zinazoshirikiana nao katika mapambano dhidi ya virusi vya Ukimwi wakiwamo GGM ambao kwa miaka 17 wamechangia fedha kupitia mradi wa Kilimanjaro HIV& AIDS Challenge, zaidi ya Dola za Marekani bilioni tano (sawa Sh. trilioni 11) kwa ajili ya kufanikisha mapambano hayo.

Habari Kubwa