Bil. 216/- zawekezwa Mfuko wa Umoja

03Dec 2019
Beatrice Bandawe
Nipashe
Bil. 216/- zawekezwa Mfuko wa Umoja

JUMLA ya Sh. bilioni 216  zimewekezwa katika  Mfuko wa Umoja (Umoja Fund) na wawekezaji nchini  kupitia Kampuni ya  Uwekezaji ya UTT AMIS  kuanzia Mei 2005 ulipozinduliwa hadi Juni  mwaka huu.

Mkurugenzi wa Uwekezaji wa Mfuko wa Umoja,  Pamela Nchimbi

Hayo yalisemwa na  Mkurugenzi wa Uwekezaji wa Mfuko wa Umoja,  Pamela Nchimbi, katika mkutano mkuu wa mwaka uliwashirikisha wawekezaji kutoka maeneo mbalimbali nchini ili kupata taarifa kuhusu mifuko yote ya UTT AMIS inavyoendeshwa, kupata taarifa za hesabu na kujadili changamoto zilizopo katika uendeshaji na namna ya kuzitatua.

Alisema  Mfuko wa  Umoja  ni mfuko wa kwanza kuanzishwa na UTT AMIS, mfuko umeendelea kufanya vizuri  kwa miaka 14 mfululizo.

Katika kipindi cha miaka minne mfululizo kuanzia Juni 2015 hadi Juni, 2019, ukubwa wa Mfuko wa Umoja umekuwa ukipanda na kushuka.

Juni 2019, ukubwa wa Mfuko wa Umoja uliongezeka kwa Sh. bilioni nne kutoka Sh. bilioni 212 kama ilivyokuwa Juni 2015 hadi  Sh. bilioni 216, Juni 2019.

Vile vile, thamani ya kipande  (NAV) iliongezeka hadi Sh. milioni 576.92 kutoka Sh. milioni 455.50 mnamo  Juni  2015 ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 27.00 .

Akielezea faida ya mfuko, alisema faida kwa  miaka minne kwa wastani ilikuwa asilimia 6.44.

Mwaka 2016  faida ilikuwa asilimia sita, mwaka 2017 faida ilikuwa asilimia 6.6, mwaka 2018 faida ilikuwa asilimia 14.45 na mwaka 2019 faida ilishuka mpaka asilimia 1.29.

Mpaka sasa faida jumuishi ya mfuko tangu kuanzishwa ni asilimia 13.42, ingawa kumekuwapo na changamoto kadha katika soko la hisa.

Kupanda na  kushuka kwa faida na thamani ya kipande cha Mfuko wa Umoja imesababishwa na mdororo  katika soko la hisa.

“Mwekezaji yeyote anayetaka kuwekeza kupitia mfuko wa Umoja, unaruhusu mwekezaji wake kuuza  vipande kwa wakati wowote, hivyo kumpa fursa mwekezaji kupata faida anapozihitaji na hakuna kiwango cha chini cha uwekezaji kinachoruhusu kupata faida,” alisema Pamela.

Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya UTT AMIS,  Casmir Kyuki, alisema ili kuwahudumia wawekezaji kwa njia rahisi zaidi na kupanua wigo kwa wawekezaji, UTT AMIS imezindua mfumo mpya wa Tehama unaojulikana kama ‘UTT AMIS APP’  ili  kusaidia wawekezaji kununua vipande kwa njia ya simu badala ya kwenda katika ofisi za UTT AMIS kupata huduma.

“Kupitia mfumo huu mwekezaji ataweza kutumia simu kiganjani (mobile devices) kupata taarifa za bei ya kipande, kununua kipande kwa simu ya kiganjani,  taarifa za uwekezaji, taarifa zote za mifuko ya UTT AMIS,  thamani ya kipande cha mfuko wowote na pia kupata taarifa fupi ya akaunti yako (last five transactions)  ikiwemo uwekezaji wako,” alisema.

Ili kupata huduma hii kupitia UTT AMIS APP,  mwekezaji  lazima ajiunge na huduma ya simu  ili aweze kupata huduma hii kwenye kiganja.

Alieleza kuwa kupitia mfumo huu wawekezaji wanaotumia mtandao wa Tigo-Pesa, M-Pesa, Airtel Money, T-Pesa, Halopesa wataweza kununua vipande kupitia simu zao.

Vile vile, maboresho zaidi yanaendelea ili kuwawezesha watumiaji wa simu za kisasa (smart phone) kupata huduma  kwa urahisi zaidi na kwa kuanzia mifumo ya UTT AMIS, imeunganishwa na mifumo ya benki ya CRDB ambayo pia ni msimamizi wa mifuko.

Faida katika mfuko imekuwa juu ya kigezo linganishi ikiwa ni wastani wa faida ya asilimia kuni kwa miaka mitano iliyopita.

Pia katika kipindi hicho chote thamani ya mfuko imeendelea kukua pamoja na idadi ya wawekezaji kuongezeka kutokana na kuongezeka kwa imani na uelewa kuhusu mifuko ya uwekezaji wa pamoja.

Habari Kubwa