DC Sabaya arejesha eneo la Tanesco baada ya miaka 35

03Dec 2019
Na Mwandishi Wetu
HAI
Nipashe
DC Sabaya arejesha eneo la Tanesco baada ya miaka 35

MKUU wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya, ameamuru kukamatwa na kuhojiwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), ofisa mstaafu wa Jeshi la Wananchi (JWTZ)-

-Kapteni John Mushi, baada ya kudaiwa kujimilikisha isivyo halali kiwanja cha Shirika la Umeme (Tanesco) kwa miaka 35.

Imedaiwa kuwa wakati ofisa huyo akimiliki kiwanja hicho kilichoko eneo la Bomang’ombe wilayani humo, Tanesco ilikuwa inalipa kodi ya pango la ardhi ambayo kwa kipindi chote ni Sh. milioni 20.

Akiwa ameongozana na kamati yake ya ulinzi na usalama jana, Ole Sabaya alipofika katika eneo hilo, aliamuru ofisa huyo kuwekwa chini ya ulinzi wa Jeshi la Polisi kisha kumkabidhi kwa Mkuu wa Takukuru Wilaya ya Hai kwa ajili ya mahojiano ya namna alivyokipata kiwanja hicho.

“Miaka hiyo ya 1980 wakati mzee huyu (Kapt. Mushi) akiwa Mkurugenzi wa Fiber Board (bodi ya samani zitokanazo na mbao) ambayo ni taasisi ya serikali, walikuwa wakinunua magogo kutoka West Kilimanjaro.

"Kwa sababu hili ni eneo la wazi na ni eneo la umma, wakawa wanayaweka hapa. Mmenielewa? Huyu akiwa DG (Mkurugenzi Mkuu) kama ambavyo ninyi Tanesco leo mnavyoweza mkaweka nguzo katika eneo lolote la umma, ndiyo kilichokuwa kinafanyika.

“Mwaka 1982, hiyo Fiber Board ikabinafsishwa ikarudi kuwa mikononi mwa wale waliochukua, ikawa sehemu ya wamiliki ni taasisi binafsi.

"Huyu akijua kwamba hili ni eneo la umma na akijua kwamba walikuwa wanaweka magogo yao hapa, akaendelea kulihodhi hili eneo.

"Kwa hiyo, ninyi mlivyokuja kupewa Tanesco pale ukubwa wake wa jumla ilikuwa ni mita za mraba 7,271, lakini Tanesco wana 3,900, akabaki na mita za mraba 3,371," alidai.

Kwa mujibu wa Ole Sabaya, hakuna mtu yeyote aliyempa ofisa huyo mstaafu eneo hilo na wala hana barua ya uthibitisho wa kumiliki eneo hilo.

“Sikia Mushi, huna 'offer' (barua ya toleo), acha kutukoroga, huna barua uliyoandika kwa mkurugenzi yeyote ya kuomba eneo na hii unajua kabisa ni mali ya umma, lakini kwa makusudi toka mwaka 1984 umeihodhi kinyume cha utaratibu.

"Na wewe watu wanakufuata, Tanesco wanakuambia uwape eneo lao unawatishia, unasema wewe ni kapteni wa jeshi mstaafu, unasema mtu yeyote akitaka kujua ukichaa wako, aje hapa aingilie. Sasa, Tanesco hamna kichaa, nimekuja mimi kichaa mwenzako hapa.

“Takukuru huyu nawakabidhi hapa sasa hivi, fedha ya serikali yote ambayo unajua imepotea kutokana na wewe kulikalia eneo hili kimabavu ni jambo la kwanza naitaka.

"Jambo la pili, Tanesco kuanzia sasa hivi, nataka muondoe mali yote na msimamie uondoaji wa kila kitu hapa na vipelekwe pale maeneo ya halmashauri mpaka tutakapopata mali yetu ya serikali. Jambo la tatu, umeisababishia serikali hasara kwa miaka 35," alisema.

Kutokana na maagizo hayo ya Ole Sabaya, bidhaa zilizokuwa kwenye eneo hilo, mashine za kufyatulia matofali kwa umeme na vifaa vya ujenzi zilibebwa kwa malori na kupelekwa ofisi za halmashauri.

Ilidaiwa kuwa vifaa hivyo ni mali ya mfanyabiashara wa Sanya Juu wilayani Siha, Kedimond Ollotu, aliyekuwa amekodi eneo hilo kwa ajili ya shughuli zake za biashara ya vifaa vya ujenzi.

Habari Kubwa