Mwakinyo amrudia Matumla, ashukiwa

03Dec 2019
Shufaa Lyimo
Nipashe
Mwakinyo amrudia Matumla, ashukiwa
  • ***Ruta, Abdallah 'Ustadhi' wamponda, atakiwa kuiga uungwana na uanamichezo wa Samatta, mwenye...

WADAU mbalimbali wa mchezo wa ngumi wamemtaka bondia, Hassan Mwakinyo, kumwomba radhi bondia mkongwe hapa nchini, Rashid Matumla "Snake Boy" kutokana na kitendo chake cha kumponda kutokana na uchambuzi aliokuwa akiufanya wakati wa pambano lake dhidi ya Mfilipino Arnel Tinampay likiendelea.

Licha ya Mwakinyo kujirekodi na kusikika katika mitandao mbalimbali akimkashifu Matumla, baada ya mkongwe huyo kutoa maoni yake wakati pambano likiendelea Ijumaa iliyopita na muda mfupi baada ya kutangazwa kuibuka na ushindi, bado alisikika kupitia redio moja jijini Dar es Salaam akiendelea kumponda mkongwe huyo.

Kupitia redio hiyo, Mwakinyo alisema Matumala alipewa nafasi hiyo ya uchambuzi ili apate hela ya kula, lakini ameitumia vibaya na kuwafanya watu wakiwamo mashabiki wake wengi kutoka kwao mkoani Tanga kuamini kwamba alibebwa dhidi ya Mfilipino huyo.

"Siku nyingine Azam Tv wakiandaa pambano wasimtumie Matumla kama mchambuzi, amefanya wengi waamini nilibebwa, kwanza kamkosea sana kocha wangu," alisema Mwakinyo.

Katika sehemu ya uchambuzi wa Matumla wakati pambano hilo likiendelea, alisema Mwakinyo anapaswa kutomruhusu Tinampay kumpeleka hadi kwenye kamba, lakini asikubali kushambuliwa sana tumboni na kwenye mbavu maana itamsababishia kupoteza nguvu.

Aidha, Matumla aliendelea kuchambua kuwa, hadhani kama kocha wa Mwakinyo alifuatilia ipasavyo namna mpinzani wake huyo, Tinampay anavyocheza na kuweza kumwandaa vema bondia wake kuelekea pambano hilo lililofanyika katika Uwanja wa Uhuru.

Hata hivyo, Matumla alivyotakiwa kujibu hoja ya Mwakinyo, alisema kama bondia huyo ametaka kuombwa radhi basi yeye anamwomba radhi na hataki malumbano katika hilo kwa kuwa alichokifanya ilikuwa ni uchambuzi na si vinginevyo.

"Kama anataka nimwombe radhi basi namwomba, yeye ni mfalme anataka kuwa mfalme muache awe mfalme," Matumla alijibu kiungwana.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Chama cha Ngumi za Kulipwa Tanzania (PST), Anthony Ruta, amesema Mwakinyo yeye ndiye anatakiwa amwombe radhi Matumla kutokana na kumkosea mkongwe huyo, kwa sababu alichokizungumza ni kwa ajili ya kumjenga na si "kumponda" kama ambavyo inadaiwa.

Ruta alisema kuwa hajafurahishwa na maneno aliyoyatoa Mwakinyo, na kuongeza kwamba bado ni bondia anayekua hivyo anahitaji kusikiliza ushauri kutoka kwa mabondia wengine waliomtangulia.

"Kiukweli sijafurahishwa na maneno aliyoyatoa Mwakinyo, cha msingi amtafute Matumla amuombe radhi kwa matokeo yote yasiyopendeza ambayo ameyasema," alisema Ruta.

Yassin Abdallah "Ustadhi", mratibu wa mapambano mbalimbali ya ngumi nchini, alisema Mwakinyo hakupaswa kutoa "maneno machafu" kwa Matumla hata kama angeshindwa pambano hilo.

"Mimi nashauri Mwakinyo amtafute Matumla kwa lengo la kumuomba radhi, yeye bado safari yake ndio imeanza, Matumla ni mkongwe na amepigana zaidi ya mapambano 50, hata kama nyota yake imeng'aa mapema ni bahati, hapaswi kumtukana Matumla," alisema Ustadhi.

Wadau wengi waliochangia mada hiyo walisema Mwakinyo anapaswa kuiga uungwana kama wa mshambuliaji na nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta ambaye baada ya kukosolewa sana kuwa aliboronga katika mechi mbili za kuwania kufuzu Afcon 2021 dhidi ya Equatorial Guinea na Libya alijibu kiungwana.

"Awe mwanamichezo kama Samatta, tazama alivyokubali kukosolewa na kusema ameyapokea maoni ya Watanzania na kuahidi kuyafanyia kazi, huo ndio uanamichezo na si kubishana na wachambuzi na mashabiki," alisema Juma Mmary.

Hashimu Kondo, yeye alisema: "Hata Messi [Lionel] wa Barcelona, huwa anakosolewa sana anaposhindwa kuisaidia Argentina, lakini kamwe humsikii akibishana na wachambuzi na mashabiki, halafu huwezi kusema mashabiki wako wa Tanga, wakati waliokuwa wakikushangilia ni Watanzania wote.

"Uwanja wa Uhuru ulitapika, atasemaje Matumla amewakwaza mashabiki wake wa Tanga, ambao walikuja ni 'vi-Costa' vitatu, huyu naona bado ana utoto sana ajifunze namna ya kuwateka mashabiki."

Aidha, Chaurembo Palasa, ambaye alikua jaji wakati wa pambano la bondia huyo kutoka jijini Tanga, alisema Mwakinyo alipata ushindi wa halali na anawataka Watanzania kuacha kuongea mambo ambayo si ya kweli.

"Mwakinyo alishinda kihalali, katika mchezo wa ngumi pointi unapata unapompiga mpinzani wako ngumi za madhara, na kupiga ngumi nyingi zisizo na madhara si sababu," alisema Palasa.

Habari Kubwa