DC Sabaya amkosha RC Mghwira mapato

04Dec 2019
Na Mwandishi Wetu
HAI
Nipashe
DC Sabaya amkosha RC Mghwira mapato

MKUU wa Mkoa wa Kilimanjaro, Dk. Anna Mghwira, amempongeza Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya, kwa kubuni na kuboresha vyanzo vya mapato wilayani humo.

Dk. Mghwira alitoa pongezi hizo jana alipozungumza na watumishi wa halmashauri ya wilaya hiyo, akisisitiza kuwa halmashauri yoyote haiwezi kujiendesha pasi na mapato.

Alitaja baadhi ya maeneo ambayo serikali wilayani humo imeboresha kuwa ni pamoja na upatikanaji wa mapato katika eneo la utalii la chemchemi ya maji moto, maarufu Chemka na stendi kuu ya mabasi Bomang'ombe.

Akiwa katika Kijiji cha Mijongweni, Dk. Mghwira aliwataka maofisa kilimo na mifugo wa wilaya kupiga kambi ya siku 15 kijijini huko ili kuwaelimisha wananchi namna bora ya kulima kilimo chenye tija na ufugaji wa kisasa.

Ole Sabaya kwa upande wake, aliwatahadharisha viongozi wa serikali ya kijiji hicho kuhusu matumizi ya mali za wananchi.

Katika taarifa yake kwa Dk. Mghwira, Ole Sabaya alikitaja kijiji hicho kuwa ni kati ya vilivyopokea fedha za miradi mikubwa ukiwamo wa Sh. milioni 200 zilizotolewa na Shirika la Maendeleo ya Japan (JICA).

Awali, akitoa taarifa ya halmashauri, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai, Jacob Muhumba, alimweleza Dk. Mghwira kuwa halmashauri hiyo ipo mstari wa mbele kutekeleza maagizo ya mkoa katika kuwahudumia wananchi.

Habari Kubwa