Waona fursa ya utalii kuhimiza umoja Afrika

04Dec 2019
Woinde Shizza
MOSHI
Nipashe
Waona fursa ya utalii kuhimiza umoja Afrika

WADAU sekta ya utalii kutoka nchi za Uganda, Zimbabwe na Tanzania wamewashauri Watanzania kujenga utamaduni wa kutembelea vivutio vikubwa vya utalii vilivyopo barani Afrika kama njia mojawapo ya kuunga mkono utalii wa ndani.

Wamesema kuna haja makundi ya vijana katika nchi zao kutumia vivutio hivyo kama njia ya kuhamasisha umoja wa Afrika na ushirikiano katika nyanja muhimu za maendeleo ikiwamo fursa za utalii.

Wakizungumza baada ya safari ya siku sita ya kuelekea kwenye kilele cha Mlima Kilimanjaro, wajumbe watatu kutoka nchi za Uganda, Tanzania na Zimbambwe, walisema licha ya mlima huo kuwa katika orodha ya maajabu saba ya dunia na kuwa mlima mrefu kupita yote barani, bado vijana wengi hawajautembelea.

Emanuel Motta, mhamasishaji kutoka Tanzania ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Origin Trail, alisema lengo la kupanda mlima huo ni kuhamasisha vijana kutoka nchi zote 55 za Bara la Afrika, kupanda mlima huo ili kutimiza agenda ya Afrika Tunayoitaka 2063 pamoja na kutimiza Malengo Endelevu ya Umoja wa Mataifa.

"Mei mwakani, tutakuwa na tukio kubwa la vijana kutoka nchi zote za Afrika watapanda Mlima Kilimanjaro, hii ni fursa tunaomba vijana waungane na sisi, wako watakaopanda kwa miguu na wengine watatumia vyombo vya usafiri.

Mkurugenzi wa Great Africa Art Banner kutoka Zimbabwe, Munyaradzi Muzenda, alieleza kufurahishwa na vivutio vilivyoko katika mlima huo ambao mtu yeyote akifanikiwa kuupanda na kulifa kileleni ni ishara ya ushujaa na kuvishinda vikwazo katika upandaji wa mlima na maisha kwa ujumla.

Muzenda alisema wanahamasisha vijana kuchora mabango makubwa ya Afrika Tunayoitaka na kupeleka mabango hayo katika kilele cha mlima huo.

Mkurugenzi wa Sister Organization, Ayaa Musuya, kutoka Uganda, alisema mlima huo utatumika kama kiunganishi kwa vijana wa Bara la Afrika kwa kuwaleta pamoja na kuweka mpango wa pamoja na kutekeleza agenda za Afrika Tunayoitaka.

Habari Kubwa