Uwekezaji Saut wamkuna waziri

04Dec 2019
Nebart Msokwa
MBEYA
Nipashe
Uwekezaji Saut wamkuna waziri

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako, amesema serikali itaendelea kushirikiana na taasisi binafsi vikiwamo vyuo vikuu vinavyomilikiwa na taasisi za dini katika kuboresha sekta ya elimu.

Ndalichako alisema hayo jijini hapa alipokuwa anazindua majengo ya kisasa ya ofisi za wahadhiri na hosteli za wanafunzi wa Chuo cha Mtakatifu Augustine (Saut) Tawi la Mbeya na alifurahishwa na uwekezaji wa chuo hicho.

Alisema uwekezaji unaofanywa na chuo hicho kwenye miundombinu ina tija na ni moja ya utekelezaji wa vitu ambavyo serikali inasisitiza katika kuweka mazingira bora ya utoaji elimu kwa Watanzania.

Sekta binafsi, alisema ni muhimu sana katika kuwaletea maendeleo na kwamba ndio maana serikali inashirikiana na taasisi binafsi kwenye utekelezaji wa mambo mbalimbali yakiwamo maendeleo ya elimu ambayo alisema ni sekta muhimu.

"Uwekezaji wenu ni wa hali ya juu sana. Nawapongeza kwa kazi nzuri na niwahakikishie kwamba serikali itaendelea kushirikiana nanyi kwa sababu mambo mnayoyafanya yanaonekana. Mnatekeleza yale ambayo tunayahitaji kwa ajili ya Watanzania," alisema Prof. Ndalichako.

Alisisitiza kuwa serikali inataka mazingira ya kutolea elimu yawe bora na miundombinu iliyopo ni sehemu ya mazingira yanayotakiwa.

Pia alisema chuo hicho kimeweka mazingira bora kwa ajili ya watoto wa kike kwa madai kuwa hosteli zilizojengwa zitawasaidia kutoka jirani na mazingira ya chuo badala ya kutoka maeneo ya mbali ambako watakuwa wanatumia muda mwingi kusafiri.

Mkurugenzi wa Saut Tawi la Mbeya, Prof. Romuald Haule, alisema jengo la ofisi ya wahadhiri limegharimu Sh. milioni 800.8 kukamilika na jengo la hosteli ya wasichana imegharimu Sh. bilioni 1.531.

Alisema hosteli iliyojengwa chuoni hapo kwa ajili ya wasichana, ina uwezo wa kuchukua wanafunzi 420 kwa wakati mmoja na huduma zote muhimu zinapatikana na hivyo wanafunzi hawatalazimika kwenda nje wakati wa usiku.

Habari Kubwa