Utafiti mafuta, gesi wafikia pazuri

04Dec 2019
Rahma Suleiman
ZANZIBAR
Nipashe
Utafiti mafuta, gesi wafikia pazuri

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imesema matokeo ya utafiti wa nishati ya mafuta na gesi bado haujakamilika na uko katika hatua za mwisho za kusoma mistari ya picha zilizopigwa.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Nishati, Salama Aboud Talib, alisema hayo jana wakati akitoa ufafanuzi kuhusu hoja za wajumbe wa Baraza la Wawakilishi waliotaka  kupewa taarifa za matokeo ya utafiti wa mafuta na gesi.

Salama alisema mkataba wa mgawanyo wa mafuta na gesi ulitiwa saini Novemba 23, mwaka jana, na baada ya hapo kazi ya utafiti ilianza mapema.

Alisema kampuni ya Rakgas kutoka Rasilkhema iliipa kazi ya kufanya utafiti kampuni ya BGC kutoka China kwa kupiga picha za angani na kufanya mitetemo ardhini na baharini.

Kwa mujibu wa waziri, kazi inayofanyika ambayo inahitaji uangalizi wa hali ya juu ni kutafsiri mistari ya picha zilizopigwa katika maeneo mbalimbali vikiwamo vitalu vya mafuta vilivyoko Unguja na Pemba.

Alisema serikali inafuatilia kwa karibu sana utafiti huo na matokeo yake yatakapokuwa tayari wananchi watajulishwa.

“Hivi karibuni nilikuwa Malaysia kwa ajili ya kufuatilia matokeo ya utafiti wa mafuta na gesi kazi iliyofanywa na kampuni ya BGC kutoka China,” alisema.

SMZ kwa kushirikiana na Rakgas kutoka Rasilkhema zimeingia makubaliano ya kufanya utafiti wa nishati na gesi katika vitalu vilivyoko Unguja na Pemba.

Habari Kubwa