Samatta njia nyeupe EPL

04Dec 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Samatta njia nyeupe EPL
  • ***Wakala wa Mo Salah amchukua, ni baada ya kuachana na yule wa awali kwa kushindwa...

NAHODHA wa timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) na klabu ya KRC Genk, Mbwana Samatta, sasa njia ni nyeupe kwake kuelekea kucheza soka Ligi Kuu England baada ya kuamua kumtema wakala wake, Margareth Byrne, kutokana na kushindwa kufanikisha dili hilo la kukipiga EPL.

Aidha, ili kufanikisha mpango huo wa kutua EPL, Samatta tayari amepata wakala mpya, ambapo sasa yupo chini ya Spocs Consulting, ambao pia wanamsimamia Mchezaji Bora wa Mwaka wa Afrika, Mohamed Salah wa Liverpool na beki wa pembeni wa zamani wa Chelsea, Baba Rahman, hao wakiwa ni miongoni tu kati ya wengi.

Mabadiliko hayo yamefanywa rasmi kupitia tangazo kwenye mitandao ya kijamii katika akaunti ya Spoc ambayo ilisomekaa 'Kila la heri kutoka Genk na karibu Mbwana Samatta kwa SPOCS'.

Huyo anakuwa wakala wa tatu kwa Samatta, 26, ambaye hivi karibuni aliichezea klabu ya Simba na kisha TP Mazembe ya DR Congo kabla ya kutua Genk.

Awali alikuwa chini ya Sportback Football, inayomilikiwa Nicolas Onisse ambao walifanikisha mpango wake wa kujiunga na KRC Genk.

Na kisha Samatta akaachana na wakala huyo na kujiunga na First For Players mwishoni mwa mwaka uliopita lengo likiwa ni kutaka kutekeleza ndoto yake ya kwenda kucheza Ligi Kuu England.

Byrne, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa zamani wa Sunderland, ambaye Samatta amemtema kwa sasa, ndiye wakala wake wa mwisho kabla ya kuamua kuwa chini ya Spocs Consulting, akitarajia kukamilisha ndoto zake za kucheza EPL kuelekea dirisha la usajili la Januari.

Samatta alikuwa na matumaini ya kukamilisha uhamisho wake wa kutoka Genk kwenda moja ya klabu za England Agosti mwaka huu, kufuatia kuwa na msimu mzuri kwenye Ligi Daraja la Kwanza Ubelgiji, lakini mpango huo ulishindikana.

Msimu uliopita aliiwezesha KRC Genk kutwaa ubingwa huku akitwaa tuzo ya Ebony Shoe, inayotolewa kwa mfungaji bora wa Afrika anayecheza Ubelgiji.

Katika mafanikio yake, pia aliiwezesha Tanzania kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) 2019 nchini Misri ikiwa ni mara ya kwanza kwa Taifa Stars kushiriki baada ya miaka 39.

Amefunga mabao 20 na kutoa pasi za mwisho sita katika mashindano yote kwa klabu na taifa hadi sasa, huku akitajwa kuwa miongoni mwa wachezaji wanaowania tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka wa Afrika 2019.

Habari Kubwa