Zahera aitwa Yanga, Mwandila kufunguka

04Dec 2019
Shufaa Lyimo
Nipashe
Zahera aitwa Yanga, Mwandila kufunguka

WAKATI Uongozi wa Yanga, ukimuita mezani aliyekuwa Kocha Mkuu wa klabu hiyo, Mwinyi Zahera ili waweze kumalizana, aliyekuwa msaidizi wake, Noel Mwandila amesema kesho naye atafunguka mpango mzima kabla ya kusepa zake Zambia.

Akizungumza na Nipashe jana, Makamu Mwenyekiti wa Klabu ya Yanga, Frederick Mwakalebela alisema, pesa wanazodaiwa na Zahera ni za kawaida sana, hivyo watazilipa bila kuwapo kwa vikwazo vya aina yoyote kwa kuwa kwanza ni haki yake kulipwa.

"Zahera tutamlipa pesa zake kwa sababu ni pesa za kawaida ambazo zinalipika kirahisi naamini kila kitu kitakwenda sawa, yeye aje tu klabuni maana tunasikia yupo jijini lakini hatujaonana.

"Siwezi kuweka hadharani kiasi cha pesa anachodai Zahera kwani hayo ni mambo ambayo yapo baina ya uongozi pamoja na mhusika mwenyewe," alisema Makamu huyo.

Katika hatua nyingine, msaidizi wa Zahera, Mwandila, amesema hana ugomvi na klabu hiyo na kwamba mkataba wake umemalizika jana na anatajia kurudi zake Zambia kwenda kujipanga na mambo mengine.

"Kwa sasa siwezi kusema chochote juu yangu na Yanga kwa sababu mkataba wangu unaisha leo [jana], Alhamisi [kesho] nitakuwa na mengi ya kusema, nitayaweka hadharani," alisema Mwandila.

Aidha, alisema amevutiwa na upendo pamoja na umoja walionao Watanzania katika kipindi chote alichokaa hapa nchini.

Habari Kubwa