Mfumo wadhibiti mimba gerezani

04Dec 2019
Joseph Mwendapole
Dar es Salaam
Nipashe
Mfumo wadhibiti mimba gerezani

MFUMO madhubuti uliowekwa katika magereza mbalimbali nchini umefanikisha kudhibiti mimba kwa wafungwa na mahabusu.

Mrakibu Mwandamizi wa Jeshi la Magereza nchini, Amina kavirondo

Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Mrakibu Mwandamizi wa Jeshi la Magereza nchini, Amina kavirondo, kwenye kikao cha siku mbili cha tathmini ya Mpango wa Kitaifa wa Kutokomeza Ukatili wa Wanawake na Watoto (MTAKUWWA).

Mkutano huo ambao ni mwendelezo wa siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia zilizozinduliwa hivi karibuni mkoani Dodoma, umebeba kaulimbiu ‘Kizazi Chenye Usawa: Simama Dhidi ya Ubakaji’.

Amina alitoa ufafanuzi huo wakati akijibu hoja ya mjumbe wa mkutano huo aliyedai kuwa kuna wanawake wanapata mimba wakiwa magerezani.

Alisema kutokana na udhibiti huo haijawahi kutokea hata siku moja mahabusi au mfungwa akapata ujauzito akiwa kwenye gereza lolote nchini.

“Hakuna wakati ambapo kwenye gereza lolote Tanzania mfungwa au mahabusi aliwahi kupata mimba. Nina miaka 24 kazini nazungumza kitu ambacho ninauhakika nacho haijawahi kutokea na haiwezi kutokea kama mnavyodhani,” alisema.

Alifafanua kuwa mfungwa anapoingia gerezani siku ya kwanza anapimwa vipimo vingi ikiwamo ujauzito kama ni mwanamke na iwapo atabainika kuwa na mimba taarifa huwasilishwa kwa viongozi wote wa juu wa jeshi hilo.

Amina alisema kama mfungwa wa kike ataingia gerezani akiwa hana ujauzito hawezi kuupata akiwa ndani kwa kuwa wameweka utaratibu mzuri ambao hakuna nafasi kwa mfungwa huyo kuonana na mwanaume awe askari wa kiume au mfungwa wa kiume.

Akifungua mkutano huo, Ofisa Maendeleo ya Jamii kutoka Ofisi ya Rais Tamisemi, Mwajina Lipinga, alisema serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa asasi zisizo za kiserikali katika utekelezaji wa Mtakuwwa.

Alisema wakati serikali ikiandaa mpango huo ilishirikisha asasi binafsi hivyo utekelezaji wake unahitaji ushirikiano wa pande zote mbili ili kufikia malengo yake mwaka 2022 ya kupunguza ukatili huo angalau kwa asilimia 50.

Aliipongeza WiLDAF kwa namna inavyoratibu mashirika 63 kwenye utekelezaji wa mpango huo na kwamba hiyo ni dalili njema kuwa jukumu hilo halijaachwa kwa serikali pekee.

Mkurugenzi wa WiLDAF, Anna Kulaya, alisema mkakati huo ni matokeo ya kazi kubwa ya ushawishi wa asasi binafsi baada ya kuona matukio ya ubakaji na unyanyasaji wa wanawake na watoto umeshika kasi.

Alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi nne duniani zinazotelekeza mpango wa Mtakuwwa na kwamba baadhi ya nchi zitakuja kujifunza namna ilivyofanikiwa kuutekeleza na changamoto zake.

“Mpango huu usipofanikiwa haitaangaliwa serikali bali itaangaaliwa nchi hivyo sisi wadau wa asasi binafsi lazima tukae pamoja tuseme wapi tumefanikiwa na wapi kuna changamoto,” alisema.

Habari Kubwa