Jafo awapa majukumu viongozi Chamwino

04Dec 2019
Paul Mabeja
CHAMWINO
Nipashe
Jafo awapa majukumu viongozi Chamwino

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, ameutaka uongozi wa Halmashauri ya Chamwino mkoani Dodoma kusimamia upatikanaji wa vifaa vya ujenzi wa Hospitali ya Uhuru kila hatua ili ikamilike kwa wakati uliopangwa.

Jafo alitoa maagizo hayo jana alipotembelea kukagua eneo jipya ambalo litajengwa hospitali hiyo kwa kutumia fedha zilizotolewa na Rais John Magufuli ambazo zingetumika katika sherehe za maadhimisho ya Siku Uhuru wa Tanganyika Desemba 9, mwaka jana.

Aidha, alisema serikali imeamua kuhamisha ujenzi wa hospitali hiyo kutoka enao ambalo Rais aliweka jiwe la msingi, kutokana na umbali uliokuwapo mpaka eneo la barabara kuu ya Dodoma-Morogoro.

Jafo alisema lengo la hospitali hiyo ni kusaidia watu ambao watapata ajali katika barabara hiyo, hivyo kuijenga umbali ambao ilikuwapo awali hakuta kuwa na tija.

“Lengo la hospitali hii kujengwa ni kwa ajili ya kusaidia wale wanaopata ajali, wanaopata dharura za kuzidiwa wakiwa barabarani wapate huduma katika maeneo ya jirani, hivyo kule ambako tuliweka awali ni zaidi kilomita tatu kutoka barabara kuu,” alisema Jafo.

Kutokana na hali hiyo, Jafo, aliwaagiza viongozi wa Wilaya ya Chamwino ambako hospitali hiyo inajengwa kuhakikisha vifaa kwa ajili ya ujenzi huo vinapatikana muda wote ili ujenzi ukamilike kwa wakati.

“Mkuu wa wilaya pamoja na timu yako ya ofisi ya mkurugenzi hakikisheni kuwa vifaa vyote vinapatikana mkandarasi asipate shida ili kukamilisha ujenzi huu katika kipindi kilichopangwa na mimi nitakuwa napita muda wote kukagua,” alisema.

Mkandarasi wa ujenzi wa hospitali hiyo kutoka Suma JKT, Omary Jafari, alisema mradi huo unatarajiwa kukamilika Mei 25, mwakani kwa gharama ya Sh. bilioni 3.99.

Habari Kubwa