Lukuvi awavaa wakurugenzi hati ardhi

04Dec 2019
Na Mwandishi Wetu
IRINGA
Nipashe
Lukuvi awavaa wakurugenzi hati ardhi

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, amewataka wakurugenzi wa halmashauri kuanza kujitathmini katika idadi ya hati wanazotoa kwa wamiliki wa ardhi kwenye halmashauri zao.

Lukuvi alisema hayo jana katika mkutano wake wa kusikiliza na kutatua kero za ardhi kwa wananchi wa Mkoa wa Iringa kupitia programu ya ‘Funguka kwa Waziri’, uliyofanyika ukumbi wa Siasa ni Kilimo mjini hapa.

Alisema wizara yake itaanza kutangaza wilaya itakayoongoza katika upangaji, umilikishaji na utoaji hati za ardhi kwa wananchi ili kubaini hamashauri ambazo ziko nyuma katika kutoa hati za ardhi kwa wananchi.

''Mkurugenzi ajione fahari kuwawezesha wananchi kwa kupima na kuwapatia hati. Kama mkurugenzi huwezi kutoa hati miliki hata 100, basi wewe hufai,” alisema.

Kwa mujibu wa Lukuvi, kumilikisha na kumpatia mwananchi hati ya ardhi ni kumwezesha kiuchumi kwa kuwa anaweza kuitumia kwenye shughuli za kimaendeleo na kusisitiza kuwa wakurugenzi wa halmashauri wahakikishe wanapanga na kuwamilikisha maeneo wananchi.

Lukuvi pia alisema kwa sasa wizara yake imejipanga kuhakikisha inasogeza huduma za ardhi karibu na wananchi kwa kuanzisha ofisi za mikoa zitakazokuwa na watendaji wote wa sekta ya ardhi kama vile wapimaji, wathamini, wataalamu wa mipango miji na wasajili.

''Sasa wapimaji, wathamini na wapangaji watakuja hapa Iringa. Muundo unaanza mwezi ujao lengo ni kuwapunguzia usumbufu wananchi katika kupata huduma za ardhi,” alisema.

Waziri alisema katika kuboresha huduma za sekta ya ardhi, wizara yake itatumia mifumo unganishi itakayorahisisha utendaji kazi kwa wataalamu wa sekta ya ardhi. Kazi kubwa, alisema itakuwa ikifanyika kielektroniki badala ya kutumia makaratasi aliyoaeleza kuwa wakati mwingine husababisha tamaa kwa maofisa ardhi.

Alitolea mfano Mkoa wa Dar es Salaam kuwa umeshaanza kutumia mfumo unganishi na sasa wamiliki wa ardhi katika mkoa huo wanapatiwa hati za kielektroniki na kubainisha kuwa lengo la kuwa na mfumo unganishi ni kuondoa urasimu na kurahisisha utendaji kazi.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Hapi, alisema mkoa wake umejitahidi kupunguza kero na migogoro ya ardhi iliyokuwapo miaka ya nyuma kwa kuanzisha utaratibu wa kuwafuata wananchi kwenye maeneo yao kupitia programu ya Iringa Mpya.

Alimweleza Waziri Lukuvi kuwa, kama angekuja mwaka mmoja na nusu uliopita, basi ukumbi aliofanyia mkutano wa ‘Funguka kwa Waziri’ ungekuwa umejaa wananchi wenye kero lakini jitihada za mkoa wake zimesababisha mkutano huo kutokuwa na idadi kubwa ya wananchi wenye migogoro ya ardhi kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.

Habari Kubwa