Ubakaji, ulawiti vyashika kasi Dar

04Dec 2019
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
Ubakaji, ulawiti vyashika kasi Dar

JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limesema matukio ya ubakaji yameongeza kutoka 608 katika kipindi cha miezi 10 ya mwanzo ya mwaka jana hadi kufikia 719 katika kipindi kama hicho mwaka huu.

Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Sarah Msafiri

Takwimu hizo zinatoa tafsiri kwamba, kwa wastani kila siku, watu wawili wanabakwa katika jiji hilo la kibiashara.

Kamanda wa Polisi wa kanda hiyo, Lazaro Mambosasa, aliyasema hayo jana wakati wa uzinduzi wa kampeni ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia.

Kamanda Mambosasa alibainisha kuwa katika kipindi cha Januari hadi Oktoba mwaka jana, matukio ya ubakaji yalikuwa 608 mwaka jana na katika kipindi kama hicho mwaka huu, yalikuwa 719.

“Ulawiti nao umeongezeka kutoka 259 mwaka jana na kufikia 319 mwaka huu, matukio ya wizi wa watoto yamepungua kutoka 12 hadi matukio saba," alisema.Takwimu hizo za Jeshi la Polisi zinatoa tafsiri kwamba, kila siku kuna tukio moja la ulawiti jijini.

Kamanda Mambosasa alisema matukio ya utupaji wa watoto yamepungua kutoka 17 mwaka jana na kufikia 15 mwaka huu.

Alisema kesi za matukio hayo zimeongezeka, akieleza kuwa imetokana na elimu inayotolewa na madawati ya jinsia 25 yaliyoko jijini.

“Kesi 218 zimepelekwa mahakamani. Kati yake, za kubaka zilishinda 27, kulawiti zilishinda 99, kutupa watoto kesi zilizoshinda ni mbili," alisema.

Alisema kesi za ubakaji 19 zilishindwa kutokana na ushahidi hafifu, kesi 12 za ulawiti na mbili za utupaji watoto, pia zilishindwa kutokana na sababu hiyo.

Kamanda Mambosasa alisema kwa mwaka huu, watuhumiwa 298 walikamatwa kwa makosa ya kubaka, 133 kwa kulawiti, wanne kwa kutupa watoto na mmoja kwa wizi wa watoto. Alisema kati ya watuhumiwa waliokamatwa, wanawake ni wanne.

Kamanda Mambosasa aliwataka wananchi katika kipindi cha Siku 16 za Kupinga Ukatili, wafike vituo vya polisi ili kuhudumiwa na kuleta mabadiliko ndani ya jamii.

WANAUME WANAOPIGWA

Alisema wanawake na wanaume walioko katika uhusiano, kila mmoja ana wajibu wa kumheshimu mwenza wake ili kuzuia matukio ya ukatili wa kijinsia.

“Na ninyi wanaume, ikitokea umefanyiwa kitendo cha ukatili na mwenza wako, usisite kutoa taarifa,” alishauri.

Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Sarah Msafiri, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika kampeni hizo, aliwataka wanaume ambao wanapigwa na wake zao, wasiogope kutoa taarifa kwenye madawati hayo ya jinsia kwa kuwa hayajawekwa kwa ajili ya wanawake na watoto peke yao.

“Unakuta askari anapigwa, lakini anaogopa kuripoti au mtu mwenye misuli mikubwa anapigwa na mke wake, anaona aibu, mjitokeze kwa sababu matukio ya ukatili wa kijinsia huwaathiri zaidi watoto, mwisho wa siku wanakimbia familia zao kutokana na kuyashuhudia.

“Kama mtaogopa kwenda kwenye madawati haya ambayo wanaosikiliza hizo kesi ni wanawake, mje hata kwetu," alisema.

Msafiri aliwataka wazazi kutowahusisha watoto wakati wa kutatua migogoro yao ikiwa ni mbinu ya kuepuka kuwaathiri kisaikolojia.

Pia aliwataka madereva wa bajaji, daladala, pikipiki na utingo kuwa sehemu ya kutoa taarifa ya matukio ya ukatili wa kijinsia yanapotokea mitaani.

Habari Kubwa