Mnyika adai kumlalamikia Mkurugenzi NEC

04Dec 2019
Hellen Mwango
Nipashe
Mnyika adai kumlalamikia Mkurugenzi NEC

SHAHIDI wa nne katika kesi ya uchochezi inayowakabili viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mnyika amedai mahakamani kwamba Februari 16, 2018 aliwasiliana na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa-

-Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Ramadhani Kailima, kumlalamikia kuhusu mawakala wa chama chake kunyimwa nakala za barua za usimamizi wa uchaguzi mdogo wa ubunge wa Jimbo la Kinondoni.

Mnyika ambaye ni Mbunge wa Kibamba, alitoa madai hayo wakati akijitetea dhidi ya kesi inayowakabili.

Ushahidi huo umesikilizwa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam iliyoketi chini ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.

Upande wa Jamhuri uliongozwa na Wakurugenzi wa Mashtaka Wasaidizi, Faraja Nchimbi, Joseph Pande, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon na Wakili wa Serikali Jaqline Nyantori.

Akiongozwa na Wakili wa Utetezi, Peter Kibatala, mshtakiwa huyo wa nne katika kesi hiyo, alidai kuwa Februari 16, 2018 saa tisa alasiri alikwenda viwanja vya Buibui kuangalia maandalizi ya mkutano wa kufunga kampeni kama yalikuwa yamekamilika kwa sababu viongozi wa kitaifa walikuwa wageni katika mkutano huo.

Alidai kuwa, alikuta maandalizi yote yapo sawa kasoro ilikuwa mawakala wao walikuwa hawajapata nakala za barua za usimamizi kutoka kwa msimamizi wa uchaguzi Kinondoni.

"Wabunge wawili wa Chadema, Esther Matiko na Susan Lyimo, walikuwa ofisi za msimamizi Kinondoni tangu asubuhi, nilimpigia Susan alinieleza walifika katika ofisi hizo asubuhi na kwamba mpaka muda huo wa alasiri walikuwa hawajafanikiwa alinitaka nimpigie Mkurugenzi wa Uchaguzi," alidai na kuongeza.

"Ilipofika saa tisa na dakika zake nilirudi makao makuu nilichukua jukumu la kumpigia mkurugenzi mkuu akanijibu kwamba ameshatoa maelekezo kwa msimamizi wa uchaguzi agawe nakala za barua kwa mawakala wote, lakini hawakupewa barua hizo mpaka usiku," alidai Mnyika.

Akihojiwa na Wakili Nyantori kuhusu kufukuzwa Chuo Kikuu Dar es Salaam, shahidi huyo alidai kuwa hakufukuzwa bali aliandika barua kuahirisha mwaka.

Alidai tangu ameahirisha mwaka wa masomo Chuo Kikuu mpaka leo (jana) hajarudi tena kuendelea na masomo hayo anaendelea na siasa.

Mbali na Naibu Katibu Mkuu Chadema, Tanzania Bara, Mnyika, washtakiwa wengine ni Mwenyekiti Chadema Taifa, Freeman Mbowe, Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa, Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche washtakiwa wengine ni Naibu Katibu Mkuu Taifa, Zanzibar, Mwalimu, Mbunge wa Kibamba, John Mnyika, Katibu Mkuu Taifa, Vicent Mashinji, Mbunge wa Bunda Ester Bulaya na Mbunge wa Kawe, Halima Mdee.

Wengine ni Mbunge wa Tarime Vijijini, Heche, Katibu Mkuu Taifa, Dk. Vicent Mashinji na Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko.

Washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka 13 likiwamo la kula njama, wote wanadaiwa kuwa, Februari Mosi na 16, mwaka jana, Dar es Salaam walikula njama ya kutenda kosa la kufanya mkusanyiko usio halali na kukiuka tamko kutawanyika.

Habari Kubwa