Auawa kinyama kwa kukatwa jembe

04Dec 2019
Steven William
MUHEZA
Nipashe
Auawa kinyama kwa kukatwa jembe

MTU mmoja aliyekuwa akifanya kibarua cha kulima Fadhili Rashidi (35), ameuawa kinyama kwa kukatwa na jembe shingoni.

Mtuhumiwa Joseph Lucas (kushoto), ambaye anatuhumiwa kufanya mauaji ya Fadhili Rashidi mkazi wa Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga,  akiwa chini ya ulinzi wa Polisi.

Tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia jana katika kitongoji cha Mgombezi, kijiji cha Mafere, kata ya Mkuzi wilayani Muheza ambako alikuwa anaishi.

Ofisa mtendaji wa kata ya Mkuzi, wilayani Muheza, Japhet Hayule, alisema mtuhumiwa wa mauaji hayo ni Joseph Lukas, ambaye alikuwa akiishi nyumba moja na marehemu, wote wakiwa wanafanya vibarua vya kulima.

Akizungungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa kitongoji cha Mgombezi, Athumani Hamisi, alisema vibarua hao mtuhumiwa na (marehemu) walipita nyumbani kwake saa saba usiku wakiwa wameongozana wakienda wanakoishi huku wakiwa wamelewa, lakini walikuwa wakigombana kwa kudaiana Sh. 20,000.

Alisema kuwa asubuhi walipata taarifa juu ya tukio hilo na yeye alitoa taarifa kwa mtendaji wa kijiji, Victoria Masanja, ambaye naye alitoa taarifa kwa mtendaji wa kata ya Mkuzi, Japhet Hayule.

Kufuatia tukio hilo Jeshi la Polisi wilayani Muheza linawashikilia watu watatu kutoka eneo hilo kwa uchunguzi zaidi ambao ni Lukas, Abdallah Shabani na Shabani Athumani.

Kaimu mkuu wa upelelezi wa Jeshi la Polisi Wilaya ya Muheza, aliyeomba jina lake lisitajwe gazetini aliwataka wananchi kutofumbia macho matukio kama hayo na kwamba wakiwaona watu hawaeleweki wanajihusisha katika matumizi ya dawa ya kulevya ikiwamo mirungi, bangi, madawa ya kulevya na pombe haramu ya gongo watoe taarifa kwa viongozi wao kwa kuwa hiyo ndio inaleta watu kufanya mauaji.

Alisema kuwa Jeshi la Polisi wilayani Muheza litaanza msako katika vijiji vyote wilayani humo kwa ajili kukamata madawa ya kulevya ikiwamo bangi, mirungi, pombe ya gongo huku akiwataka maofisa watendaji kuwafichua vijana wanajihusisha na vitendo hivyo wakamatwe.

Mwenyekiti wa kijiji cha Mafere, kata ya Mkuzi wilayani Muheza Haji Athumani, alisema vijana ndiyo wako mstari wa mbele kwa kutumia madawa ya kulevya.

Habari Kubwa