Tanzania kuivaa Zimbabwe fainali Copa Coca-Cola kesho

05Dec 2019
Na Mwandishi Wetu
KENYA
Nipashe
Tanzania kuivaa Zimbabwe fainali Copa Coca-Cola kesho

TIMU ya soka ya Tanzania ya vijana chini ya umri wa miaka 16, COPA Coca-Cola imeendelea kufanya vizuri katika michuano ya COPA Afrika baada ya kuwatoa wenyeji Kenya kwa penalti na kutinga fainali ambapo sasa itawavaa Zimbabwe kesho.

Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Dk. Pindi Chana (nguo nyekundu, aliyeonyesha dole gumba) akifurahia na kocha wa timu ya vijana wa Tanzania, Abel Mtweve (aliyevaa kofia) pamoja na wachezaji wa timu hiyo baada ya kuitoa Kenya kwa penalti 5-4 kwenye mechi ya nusu fainali ya michuano ya Copa Coca-Cola Afrika iliyopigwa Uwanja wa M-PESA Foundation Academy nchini Kenya jana. MPIGAPICHA WETU

Katika mechi hiyo ya nusu fainali iliyopigwa katika Uwanja wa M-PESA Foundation Academy, Thika nchini Kenya, Tanzania ilishinda kwa penalti 5-4 baada ya mchezo huo kumalizika kwa sare tasa.

Haukuwa ushindi mwepesi kwa timu ya Tanzania inayonolewa na Kocha Abel Mtweve, kwani timu ya Kenya ilipigana mpaka mwisho na kulazimisha sare mpaka kipenga cha mwisho.

Hata hivyo, vijana wa Tanzania walicheza soka safi na la kuvutia licha ya timu zote mbili kushindwa kuliona lango la mwezie mpaka dakika ya mwisho.

Kipa wa Tanzania, Chuma Ramadhani, aliibuka shujaa wa mchezo huo baada ya kufanikiwa kuchomoa penalti moja kati ya tano na kuiweka Tanzania kutinga fainali.

Penalti za Tanzania zilizamishwa nyavuni na Mohameed Rai, Edward Bernard, Nyerere Paul, Frank Stephen na Innocent Mtoi, ambapo kwa ushindi huo itakutana na Zimbabwe fainali kesho, iliyoitoa Zambia kwa kuichapa mabao 4-2 katika mchezo mwingine wa nusu fainali uliopigwa jana.

Timu ya Tanzania ilipata baraka ya kutembelewa na Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Dk. Pindi Chana ambaye aliwaongezea ari wachezaji kwa kuwasihi kuhakikisha wanashinda mechi hiyo.

Aidha, Chana aliishukuru Kampuni ya Coca-Cola kwa kuja na michuano ya namna hii yenye lengo la kuibua vipaji vya vijana kutoka katika viwango vya chini.

“Nimefurahi sana kuambiwa kuwa michuano hii inahusisha nchi kumi za barani Afrika, hivyo haya ni mashindano makubwa na yatawawezesha vijana wetu kufika mbali."

Akizungumza mara baada ya mechi hiyo kumalizika, Kocha wa Tanzania, Abel Mtweve alisema: “Mkakati wetu tangu mwanzoni umekuwa ni kushambulia kwa kushtukiza, lakini pia tunatumia muda mwingi kujilinda.”

Naye Mkuu wa Msafara, Mwalimu Vitalis Shija, ambaye ni Makamu wa UMISSETA Taifa, alitoa pongezi kwa vijana kwa kupigana hadi mwisho na kuwataka kurudi na kombe Tanzania.

Habari Kubwa