Kili Stars kuanza na Kenya, Z’bar na Sudan

05Dec 2019
Somoe Ng'itu
Dar es Salaam
Nipashe
Kili Stars kuanza na Kenya, Z’bar na Sudan

TIMU za soka za Tanzania, Kilimanjaro Stars ya Bara na Zanzibar Heroes ya Zanzibar, ambazo zinaondoka nchini leo, kuelekea Uganda kwa ajili ya kushiriki mashindano ya Kombe la Chalenji-

-yanayotarajiwa kufanyika kuanzia Jumamosi wiki hii jijini Kampala, zitaanza kutupa karata zao za kwanza Jumapili kwa kuzivaa Kenya na Sudan.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Kocha Mkuu wa Kilimanjaro Stars, Juma Mgunda, alisema kikosi hicho kimejiandaa vizuri kwenda kushindana katika mashindano hayo yanayoshirikisha nchi kutoka Afrika Mashariki na Kati.

Mgunda alisema kuwa anafahamu timu zote zinazoshiriki michuano hiyo ni nzuri na wao ndio maana wanakwenda huko kupambana ili kupata matokeo mazuri.

"Niwahakikishie tu, kuwa mimi na benchi langu la ufundi tunakwenda huko kupambana, tumejiandaa kwenda kushindana, yoyote tutakayekutana naye sisi ni changamoto," alisema Mgunda.

Naye golikipa wa timu hiyo, Aishi Manula, alisema wamefanya maandalizi mazuri na malengo yao ni kwenda kupambana ili kupata matokeo chanya katika mashindano hayo.

"Tunakwenda kupambana, kupigania nchi yetu, na timu yetu, malengo yetu kama wachezaji ni kwenda kurejesha heshima yetu, heshima ile ambayo Tanzania Bara tuliipata mwaka 2010, ni muda mrefu umepita," alisema Manula.

Wakati huo huo, Waziri wa Vijana , Sanaa, Utamaduni na Michezo wa Zanzibar, Balozi Ali Karume, amewataka wachezaji wa Zanzibar Heroes kwenda kupambana na kufanya vizuri katika michuano hiyo kwa sababu Wazanzibar wote wanawaangalia wao.

Alisema kuwa wana matumaini na timu hiyo kutokana na hamasa waliyokuwa nayo mwaka huu, ambayo ni tofauti na miaka mingine iliyopita.

“ Tunawaomba mkafanye vizuri katika michuano hiyo, kuna zawadi zenu kubwa, na hata mkifanya vibaya si kama hatutawapa zawadi, mtapewa lakini itakuwa ya kawaida ila ninamatumaini makubwa mtawapa Wazanzibar burudani inayostahili ili kuendeleza hamasa hii," alisema kiongozi huyo.

Katika hatua nyingine, Ethiopia, Sudan Kusini na wageni, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), zimeondolewa katika mashindano hayo kutokana na kushindwa kutimiza vigezo vya kushiriki michuano hiyo.

Habari Kubwa