Aussems ashukia 'vihiyo' wa Simba

05Dec 2019
Somoe Ng'itu
Nipashe
Aussems ashukia 'vihiyo' wa Simba
  • ***Aacha ujumbe mzito akitaka watimuliwe klabu isonge mbele, awalilia mashabiki, amtaja Okwi, Kotei...

ALIYEKUWA Kocha Mkuu wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Mbelgiji Patrick Aussems, ameacha ujumbe mzito kwa klabu hiyo, baada ya kuieleza kuwa ili iweze kusonga mbele, ni lazima iwaondoe viongozi "waongo" na wasio na elimu ambao wako kwenye Bodi ya Wakurugenzi.

Aussems, ametoa kauli hiyo juzi, saa chache kabla ya kupanda ndege kurejea kwao, kutokana na Simba kuamua kuachana naye kwa madai ya kufanya makosa ya kimaadili.

Mbelgiji huyo alisema anaitakia kila la kheri klabu hiyo, lakini amewakumbusha kubadilika ili kwenda na wakati.

"Asante wachezaji kwa kazi nzuri na ushirikiano tuliofanya pamoja, asante mashabiki kwa sapoti isiyoelezeka, ninawatakia kila la kheri, lakini ili Simba ikue, lazima iwaondoe viongozi waongo na ambao hawana elimu kwenye Bodi ya Wakurugenzi. Sasa ni muda wa mimi kufurahia, kitu ambacho ni muhimu katika maisha yangu na familia. Kwa kheri Tanzania," alisema Aussems.

Aliongeza kuwa baadhi ya viongozi walioko kwenye bodi hiyo, wanachangia kukwamisha maendeleo ya Simba kwa kuweka vipingamizi katika baadhi ya mipango ya klabu na kusisitiza waondolewe mapema ili kupata matokeo chanya.

Kocha huyo pia amekanusha kufanya mawasiliano na klabu ya Polokwane inayoshiriki Ligi Kuu Afrika Kusini, ikiwa ni moja ya tuhuma aliyokuwa nayo ya kuondoka kwenye kituo chake cha kazi bila ruhusa.

Mbelgiji huyo pia ameweka wazi kwamba hakuwa radhi kuona baadhi ya wachezaji aliokuwa nao msimu uliopita wakiondoka, akiwamo mshambuliaji Mganda Emmanuel Okwi na kiungo raia wa Ghana, James Kotei.

Mbali na kuipa ubingwa wa Bara, Aussems pia aliwapa Wekundu wa Msimbazi Ngao ya Jamii mara mbili huku akiwapeleka kwenye hatua ya robo fainali ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Chini ya Aussems, Simba ilipata ushindi katika mechi zake zote tatu za nyumbani za hatua ya makundi ilipowakaribisha JS Saoura ya Algeria, Al Ahly (Misri) na AS Vita kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Wakati Suleiman Matola kutoka Polisi Tanzania akiwa amerejea Simba, makocha mbalimbali wanaendelea kutajwa kuomba kurithi mikoba ya Aussems, ambaye katika mechi 10 za Ligi Kuu Bara ameshinda nane, ametoka sare moja na akufungwa mchezo mmoja wa ugenini dhidi ya Mwadui FC ya Shinyanga.

Habari Kubwa