Simba kwa Arusha, Yanga Iringa FA Cup

05Dec 2019
Adam Fungamwango
Nipashe
Simba kwa Arusha, Yanga Iringa FA Cup

WAKATI Mabingwa wa Kombe la FA, Azam FC, wakipangiwa kucheza dhidi ya African Lyon kwenye mechi za raundi ya tatu za kinyang'anyiro hicho, Mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba, watacheza na Arusha United, huku Yanga ikipambanishwa na Iringa United.

Kwa mujibu wa ratiba ya 64-bora ya michuano ya Kombe la FA iliyotolewa jana na Shirikisho la Soka nchini (TFF), ikirushwa mubashara, timu hizo za Simba, Yanga na Azam zitaanzia nyumbani, zikianza safari ya kusaka ubingwa kwa ajili ya kuiwakilisha nchi kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika (Caf).

Mechi zote za raundi hiyo ya tatu kutafuta timu 32 zitakazotinga kwenye raundi ya nne, zitachezwa kuanzia Desemba 20 hadi 22, mwaka huu. Kingine kilichovutia wengi walioshiriki kwenye droo hiyo ya upangaji wa ratiba, ni kuwapo kwa mechi kati ya Coastal Union ya Tanga dhidi ya mahasimu wao wa jadi, African Sports ambayo itachezwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.

Droo ilizidi kuvutia baada ya Pamba ya Mwanza kupangiwa kucheza dhidi ya Majimaji ya Songea, hivyo mechi zote hizo mbili kukumbusha miaka ya '80 hadi '90 wakati wa Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara ambayo kwa sasa ni Ligi Kuu.

Mechi zingine ni kati ya Lipuli dhidi ya Dar City, Kagera Sugar dhidi ya Rufiji United, Prisons ikicheza dhidi ya Mlale FC. Mtibwa Sugar nayo itakuwa nyumbani dhidi ya Rhino Rangers ya Tabora, Namungo FC dhidi ya Green Warrios, JKT Tanzania ikiikaribisha Boma FC ya Mbeya.

Biashara United itakuwa nyumbani dhidi ya Nyamongo FC zote za mkoani Mara, Mbao FC dhidi ya jirani zao Stand United, Ruvu Shooting itakuwa mgeni wa Milambo FC ya Tabora. KMC itaivaa Mbuni FC, Mwadui dhidi ya Mkamba Rangers, Alliance dhidi ya Transic Camp, Singida United itacheza na Tukuyu Stars, Polisi Tanzania dhidi ya TP Boys na Mbeya City dhidi ya Migombani FC.

Habari Kubwa