Miaka 30 jela kwa kubaka kikongwe

05Dec 2019
Juster Prudence
Nipashe
Miaka 30 jela kwa kubaka kikongwe

MKAZI wa Kijiji cha Nange mkoani Mwanza, Shabo Marando (47), amehukumiwa kutumikia kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la kumbaka bibi wa miaka 60.

Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza, Esther Malick, baada ya kupitia ushahidi wa upande wa mashtaka uliokuwa na mashahidi wanne.

Ilidaiwa na shahidi wa tatu, Dk. Judith Kiwango wa hospitali ya wilaya hiyo, aliyemfanyia uchunguzi bibi huyo kwamba, alikutwa na michubuko sehemu za siri.

Shahidi wa pili, Sama Luheka alidai alisikia kelele kichakani aliposogea alimkuta mtuhumiwa akimbaka bibi huyo.

Bibi huyo alidai mahakamani kuwa siku ya tukio, mtuhumiwa alimkuta shambani akikusanya kuni, akamkamata kwa nguvu na kumvutia kichakani kisha kumbaka.

Kwa mujibu wa taarifa ya uhalifu wa kibinadamu iliyotolewa na Jeshi la Polisi, kwa mwaka 2018, kati ya matukio 11,759, ya ubakaji yalikuwa 7,617, sawa na asilimia 64.7.

Habari Kubwa