Wazazi wadaiwa kukingia kifua watuhumiwa ubakaji

05Dec 2019
Romana Mallya
Nipashe
Wazazi wadaiwa kukingia kifua watuhumiwa ubakaji

WAKATI vitendo vya ubakaji na ulawiti vikiongezeka mkoani wa Dar es Salaam kwa kipindi cha miezi 10 ndani ya miaka miwili, wadau akiwamo Mkuu wa Wilaya Kigamboni, Sarah Msafiri, wameeleza tatizo la wazazi kuwakingia kifua watuhumiwa.

Takwimu zinaonyesha katika kipindi cha miezi 10, mwaka jana (2018) matukio ya ubakaji yaliyoripotiwa polisi jijini Dar es Salaam ni 608 na mwaka huu (2019) yameongezeka na kufikia 719 huku vitendo vya ulawiti vikiongezeka kutoka 259 mwaka jana na kufikia 319, mwaka huu.

Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Sarah Msafiri akizungumza katika Kampeni ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia, alisema ipo kesi moja ilitokea Feri, Kigamboni, jijini Dar es Salaam, mlinzi wa maduka maeneo hayo aliwalawiti watoto wa kiume.

Alisema polisi iliweka mtego uliowezesha kukamatwa kwa mlinzi huyo.

Hatua ya awali iliyochukuliwa ni kwa watoto hao kupelekwa hospitali kupimwa na ilibainika kuwa walikuwa wamefanyiwa kitendo hicho.

"Baada ya wiki mbili wale watoto walikuja ofisini na wazazi wao, mzazi ananyanyuka anatetea mtoto wake hajalawitiwa, wakati ripoti ya daktari inaonyesha amelawitiwa, tukiwa na jamii ya aina hii hatuwezi kufikia malengo,” alisema na kuongeza:

"Tutakuwa tunalilaumu Jeshi la Polisi na kuwaharibu watoto wetu kwa kutengeneza jamii ambayo siyo nzuri kwa sababu ya kutotoa ushirikiano matukio yanapotokea na kupoteza ushahidi wake," alisema.

Alisema ili kesi ziende, na haki itendeke lazima hatua za uchunguzi zikamilike kwa kila mtu kutoa ushirikiano.

"Matukio ya watoto kulawitiwa yanaendelea kuongezeka, baba acha kumlinda mke wako, mwanamke akirudi saa 12 umeshajua, mtoto akirudi saa nne usiku au hajarudi hujali, mna kazi ya kulindana wazee, wazazi mbadilike muwalinde watoto wenu," alisema.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni, alisema Mkoa wa Mjini Magharibi visiwani Zanzibar, jumla ya kesi 280 zinazohusiana na matendo ya udhalilishaji, ubakaji na ulawiti yameripotiwa.

"Tatizo hili linaendelea kukua kwa kasi na inasikitisha sana, jambo hili linachafua heshima ya nchi yetu, serikali tumeamua kuja na mkakati maalumu wa kupambana na changamoto ya udhalilishaji, ubakaji na ulawiti na tunaomba mamlaka nyingine zituunge mkono," alisema.

Naye, Mwenyekiti wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa), Joyce Shebe, akitoa maoni kuhusu kuongezeka kwa ubakaji na ulawiti, alisema lazima serikali irudi kuzungumza na wadau ili kukomboa kizazi kijacho.

"Hali hii ikiendelea hivi ilivyo kuna uwezekano mkubwa ndoa za jinsia moja huko mbeleni kuongezeka, hatua nyingine za kuchukuliwa ni upande wa ustawi wa jamii wasaidie kutengeneza mambo ya msingi ili kulinda na kutoa elimu zaidi," alisema.

Pia aliomba vyombo vya sheria vitoe ushirikiano mtuhumiwa anapokamatwa vihakikishe hukumu inatolewa.

Hata hivyo, alisema kuongezeka kwa vitendo hivyo kunachangiwa na mambo ya usasa ya mitandao ya kijamii na baadhi kujifunza na kutaka nguvu ielekezwe kwa kutoa elimu zaidi.

Juzi, Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, alitaja takwimu za ubakaji na ulawiti na kueleza kuwa katika kipindi cha Januari hadi Oktoba, mwaka jana, matukio ya ubakaji yalikuwa 608 na kufikia 719 mwaka huu.

"Ulawiti umeongeza kutoka 259 mwaka jana na kufikia 319 mwaka huu, matukio ya wizi wa watoto yamepungua kutoka 12 hadi matukio saba," alisema.

Kamanda Mambosasa alisema matukio ya utupaji wa watoto nayo yamepungua kutoka 17 mwaka jana na kufikia 15, mwaka huu.

"Kesi 218 zimepelekwa mahakamani, za kubaka zikishinda kesi 27, kulawiti zilizoshinda 99, kutupa watoto kesi ni mbili," alisema.

Alisema kesi za ubakaji 19 zilishindwa kutokana na ushahidi hafifu, ulawiti 12 na za utupaji watoto ni mbili.

Kamanda Mambosasa alisema kwa mwaka huu jumla ya watuhumiwa 298 walikamatwa kwa makosa ya kubaka, 133 kulawiti, kutupa watoto matukio manne na wizi wa watoto tukio moja.

Habari Kubwa