Chungu, tamu za Sumaye Chadema

05Dec 2019
Na Waandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Chungu, tamu za Sumaye Chadema

WAZIRI Mkuu mstaafu wa Awamu ya Tatu, Frederick Sumaye, ameelezea machungu na matamu aliyoyaonja katika siku 1,436 akiwa ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye, akizungumza na wan habari, jijini Dar es Salaam jana, alipotangaza kujivua uanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema). PICHA: MIRAJI MSALA

Mary Geofrey na Maulid Mmbaga

 

Sumaye ambaye alijiunga na Chadema Desemba 12, 2015 na kukabidhiwa kadi na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, jana alitangaza kukihama chama hicho kikuu cha upinzani kwa madai ya kukosekana kwa demokrasi.

Alitangaza msimamo wake huo rasmi jana jijini Dar es Salaam mbele ya waandishi wa habari, bila kuweka wazi atajiunga na chama gani cha siasa nchini.

Mwanasiasa huyo, Agosti 22, 2015, Sumaye alitangaza kujiondoa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa madai kuwa anaunga mkono mageuzi yanayofanywa na vyama vya upinzani vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

CHUNGU CHADEMA

Zikiwa zimebaki siku saba kabla ya kutimiza rasmi miaka minne tangu alipojiunga na Chadema, alijitokeza hadharani na kuelezea mazuri na magumu aliyopitia ndani ya chama hicho.

Alisema haikuwa rahisi kujiunga upinzani bali ilihitaji moyo kwa sababu  aliwahi kuwa na nafasi kubwa nchini na muda mfupi baada ya uamuzi huo, alianza kupata matatizo kutoka serikalini.

"Mashamba yangu yalichukuliwa na hata baadhi ya huduma zangu zilianza kuwa tofauti na wastaafu wenzangu. Familia yangu ilianza kuona mateso ya mimi kuwa upinzani na walinilaumu na kusononeka sana.

“Pamoja na hali hii ya mateso, nilikaza shingo kwa vile niliamini kuwa kinachopiganiwa na wapinzani kama kitafanikiwa ni kikubwa kuliko hiki cha familia yangu," alisema Sumaye huku akiongoze kuwa aliamini hatua aliyochukua ingejenga demokrasia ya kweli ambayo itadumisha maendeleo na haki kwa wote.

"Kwa kweli familia yangu ilishaanza kuzoea hali hiyo na hatukuwa tunagombana tena kuhusu mimi kuwa upinzani," alisema Sumaye.

Sumaye alisema jambo lingine lililomuumiza ni nongwa aliyodai kufanyiwa baada ya kuamua kuchukua fomu ya kuwania nafasi ya mwenyekiti wa taifa wa Chadema.

"Pamoja na kuwa ni haki yangu kwa mujibu wa katiba ya chama chetu, pia nilikuwa na lengo la kwanza la kuondoa hisia iliyojengeka katika jamii kuwa ndani ya Chadema hakuna demokrasia ya kweli," alisema Sumaye.

Aliendelea kueleza kuwa aliamua kuwania nafasi hiyo kuondoa dhana kuwa Chadema inamilikiwa na Mbowe peke yake na haipaswi kusogelewa na mwanachama yeyote.

"Mimi binafsi sikuamini kuwa hisia hizi ni za kweli ndiyo maana haya yasipofutika yatatuchafulia jina la chama chetu.  Kumbe mimi ndiyo nilikuwa nimekosea kufikiri hivyo. Matokeo yake badala ya busara kutumika hata kama tungetaka kumlinda Mbowe wetu, zilizotumika njia za ovyo," alisema Sumaye.

Alisema kilichotokea ni baadhi ya wajumbe wa kamati kuu ambao ndio waliofanya mpango wa kupelekewa fomu za kuwania nafasi ya Mwenyekiti wa Kanda ya Pwani, walimgeuka na kuhakikisha hashindi nafasi hiyo.

Katika uchaguzi huo, uliofanyika Alhamisi iliyopita, Sumaye alimwagwa kwa kupigiwa kura za hapana 48 dhidi ya ndiyo 28 na moja iliharibika.

"Baadhi ya wajumbe wa kamati kuu ambao ndio walifanya mpango wa mimi kuletewa fomu ya kuwania kanda hiyo, wakageuka kuhakikisha mimi ambaye nilikuwa mgombea pekee wa nafasi hiyo nanyimwa kura na za hapana zilishinda," alisema Sumaye.

Sumaye alidai wajumbe waliopiga kura wakawekwa hotelini, wakalipwa fedha kwa kazi hiyo na sababu kubwa ni kwa nini alichukua nafasi ya kuwania kiti cha mwenyekiti wa taifa.

"Basi wangenitahadharisha kuwa katika chama chetu nafasi hiyo ina utaratibu wa tofauti nje ya katiba, ningeelewa na labda ningetii na kama nisingetii basi wangenisubiri kwenye vikao vinavyohusu nafasi hiyo," alisema Sumaye na kusisitiza kuwa chama hicho hakina demokrasia ya kweli na kwamba nafasi aliyoishikilia Mbowe haiguswi.

"Kwa bahati mbaya sana ndivyo ilivyotokea na waliojaribu kuwania nafasi hiyo katika siku za nyuma yaliwakuta kama haya na labda mengine mabaya zaidi," alisema.

Sumaye alitangaza kutowania tena nafasi ya mwenyekiti taifa wa Chadema licha ya kuchukua fomu, kuilipia Sh. milioni moja, kuijaza na kuirudisha kwa wakati baada ya kufanya uchunguzi na kujiridhisha kuwa si busara kuendelea na safari hiyo.

"Inabidi leo (jana), nitangaze kuwa hiyo safari ya kugombea uenyekiti ngazi ya taifa naisitisha rasmi kwa usalama wangu, usalama wa wanachama na chama chenyewe. Kwa bahati nzuri tulipokuwa kwenye mkutano wa kanda, Mbowe alitutahadharisha kuwa sumu haionjwi kwa ulimi na mimi sitaki kuionja," alisema Sumaye.

Alisema uchaguzi wa mwaka huu ndani ya chama, umeacha majeraha ambayo si ya kushindwa kwenye uchaguzi bali mgawanyiko ndani ya chama kwa sababu watu walikuwa wanachaguana kwa kutegemea kundi la nani.

"Kwa wale waliokuwa wanaitwa timu Mbowe, kulikuwa na nguvu kubwa kutoka nje ya kanda zilizotumika na watu ambao si timu Mbowe waliumizwa sana," alisema Sumaye.

MATAMU YA CHADEMA

Sumaye alisema muda baada ya kujiunga Chadema, alipokewa vizuri na kufanya kazi kwa kushirikiana.

Alisema baada ya muda Mbowe alimteua kuingia katika kamati kuu ya chama hicho na miezi sita baadaye baadhi ya viongozi na wanachama wa Chadema wa kanda ya Pwani, walimwomba awanie nafasi ya mwenyekiti wa kanda hiyo.

Nafasi hiyo, alisema alichaguliwa na kuwa mwenyekiti hadi juzi walipofanya uchaguzi na kushindwa licha ya kutokuwa na mpinzani.

Alisema licha ya kujiondoa katika chama hicho, yuko tayari kutoa ushirikiano kama atahitajika kwa ajili ya kuwashauri juu ya yale yote yaliyotokea.

"Mwisho kabisa nataka niwaambie ndugu zangu wa Chadema mimi bado nawapenda sana na nina imani na hiki chama katika safari yetu ndefu ya kuleta mabadiliko chanya katika ujenzi wa demokrasia yetu," alisema Sumaye.

Alisema hata kama hayupo ndani ya chama hicho lakini ataendelea na kazi na kujenga demokrasia.

Naye aliyekuwa Katibu wa Kanda ya Pwani Chadema, Casmir Mabina, alitangaza kujivua nafasi hiyo kwa madai ya ‘figisu’ zilizotokea kwenye uchaguzi wa kanda hiyo.

Alisema tayari jana alikabidhi barua yake katika ofisi za makao makuu ya Chadema na atabaki kuwa mwanachama mwadilifu kupitia tawi lake.

Habari Kubwa