Serikali yatangaza msimamo uzimaji wa laini zisizosajiliwa

05Dec 2019
Na Waandishi Wetu
Nipashe
Serikali yatangaza msimamo uzimaji wa laini zisizosajiliwa

WAZIRI wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Mhandisi Isack Kamwele, ametegua kitendawili cha kuzimwa simu ambazo laini zake hazijasajiliwa kwa vidole ifikapo Desemba 31, mwaka huu, kwa kusisitiza kuwa nia ya serikali iko pale pale.

Kamwele amesisitiza msimamo huo zikiwa zimebaki siku 27 kufika siku ya mwisho ya matumizi ya laini ambazo hazijasajiliwa kwa vidole kwa kutumia vitambulisho vya taifa.

Kabla ya waziri huyo hajaweka msisitizo wa uamuzi huo jana, kumekuwapo na kauli za kukinzana baina ya viongozi wa serikali na taasisi zinazosimamia mawasiliano nchini.

Akiwa bungeni mjini Dodoma katika mkutano uliopita wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, alieleza kuwa hakuna laini ya simu ya mtu itakayofungwa kwa kukosa kitambulisho cha Taifa.

Lugola alitoa kauli hiyo wakati akijibu mwongozo wa Mbunge wa Kavuu (CCM), Dk. Pudensiana Kikwembe, ambaye alitaka kupata majibu ya serikali kuhusu wananchi ambao bado hawajapata vitambulisho vya Taifa pamoja na kusajili laini za simu.

Lugola alisema lengo la usajili na utambuzi ilikuwa ni kuwafikia watu milioni 23.3, lakini hadi sasa Watanzania milioni 20.5 wameshasajiliwa, zimezalishwa namba za vitambulisho kwa Watanzania milioni 15.5.

“Naomba niwatoe hofu Watanzania kwamba hakuna mtu yeyote ambaye laini yake ya simu itafungwa kisa hajasajili kwa sababu hana kitambulisho cha Taifa,” alisema Lugola.

Pia Lugola alisema kazi ya utambuzi, usajili na utoaji wa vitambulisho kwa wananchi ambao wana sifa za kupata vitambulisho ni endelevu na halina mwisho.

ALICHOKISEMA KAMWELE

Jana Nipashe ilimtafuta Waziri Kamwelwe kwa ajili ya kupata ukweli wa suala hilo na kuwaondolea hofu Watanzania wengi.

Kamwelwe alisema: “Kazi yangu ni kusajili laini za simu, lengo kuu likiwa ni kupunguza utapeli kwa njia ya mtandao, kuna watu wana laini 20 na ndiyo maana tumetoa muda wa kusajili.”

“Desemba 31 tutazima laini ambazo hazijasajiliwa, na ninayezima ni mimi, Waziri wa Mambo ya Ndani kazi yake ni kutoa vitambulisho vya Nida na kama alivyosema zoezi ni endelevu,” alisema Kamwelwe.

KAULI YA TCRA

Kwa upande wake, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imesema yeyote ambaye hatasajili laini ya simu kwa alama za vidole kwa mujibu wa kisheria, itafungiwa.

Hayo yalisemwa jana na Mkuu wa Kanda ya Kaskazini TCRA, Mhandisi Emelda Salum, wakati wa kampeni ya ‘Mnada kwa Mnada’ ikiwa Wilaya ya Babati mkoani Manyara.

Alisema siku zilizobaki hadi sasa ni 27 ambazo zilitolewa kwa ajili ya usajili wa laini za simu kwa alama za vidole na kuwataka wale ambao hawajafanya hivyo wajitokeze.

“TCRA ipo katika kampeni ya Mnada kwa Mnada ya uhamasishaji wa usajili wa laini za simu kwa alama za vidole ambaye hatatimiza matakwa ya kisheria ya kusajili laini ya simu kwa alama za vidole laini hiyo itafungwa," alisema Salum.

Kampeni hiyo inashirikisha kampuni ya simu, Jeshi la Polisi kitengo cha uhalifu mitandaoni, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Idara ya Uhamiaji kwa ajili ya utoaji wa huduma za usajili wa laini za simu kwa kutumia vitambulisho vya kitaifa na kuhakikiwa na kampuni za simu kwa kuweka alama za vidole kwa laini za simu.

Mhandisi Emelda alisema ni fursa kwa wananchi wa Babati na maeneo mbalimbali waliofika katika viwanja vya stendi ya zamani ya Magugu kupata namba ya kitambulisho cha Taifa na kusajili laini zao.

Alisema kampeni hiyo ilianzishwa ili kutoa fursa ya wananchi kuhudumiwa kwa pamoja na kuwataka wajitokeze kwenye maduka ya kampuni za simu kusajili laini zao kabla ya Desemba 31.

Ofisa Mawasiliano Mwandamizi wa TCRA, Mabel Masasi, alisema wananchi wameitikia wito kwa kujitokeza kuangalia namba ya vitambulisho kwa ajili ya kusajili laini zao.

Imeandaliwa na Romana Mallya na Gwamaka Alipipi

Habari Kubwa