Bayi awataka wachezaji wajitume, wasilalamike

06Dec 2019
Ashton Balaigwa
MOROGORO
Nipashe
Bayi awataka wachezaji wajitume, wasilalamike

WANAMICHEZO wa hapa nchini wametakiwa kuacha kuilaumu serikali kwa wawakilishi wake kufanya vibaya katika mashindano mbalimbali wanayoshiriki na badala yake wametakiwa kujituma na kuongeza bidii ili kufikia malengo waliyojiwekea.

Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimipiki Tanzania (TOC), Filbert Bayi

Ushauri huo umetolewa jana na Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimipiki Tanzania (TOC), Filbert Bayi, katika ufunguzi wa mkutano mkuu wa mwaka wa kamati hiyo na pia amewakumbusha wanamichezo wote kutambua kuwa michezo ni ajira na biashara.

Bayi alisema kuwa vyama vya michezo vinapaswa kuweka mazingira bora kwa wanamichezo ili waweze kufikia malengo na viwango vinavyotambulika kimataifa.

Alisema kuwa idadi ya wanamichezo wanaoshiriki Michezo ya Olimpiki kutoka Tanzania imekuwa ikipungua kwa sababu ya kukosekana kwa jitihada za mchezaji mmoja mmoja au vyama wanavyotoka.

“Sio kwamba Tanzania inashindwa kushiriki katika mashindano hayo ya Olimpiki lakini tunaendelea kupambana kuhakikisha tunaongeza kiwango cha ushiriki, kwa miaka miwili iliyopita tumeweka namba sawa sawa ya watu saba lakini inawezekana mwaka huu ikapungua tena kutokana na wachezaji wawili tu ndio waliofikia viwango,”alisema Bayi.

Kiongozi huyo alisema kuwa bado anaimani idadi ya wanamichezo watakaofikia viwango vya kushiriki Michezo ya Olimpiki itaongezeka kwa kipindi cha kuanzia Januari hadi Juni mwakani.

Hata hivyo, Bayi, alisema wamendelea kuwashawishi na kuwashauri vijana ambao wanaibukia kuwa na uzalendo katika michezo wanayoshiriki na sio kufikilia zaidi fedha na kuwaleza kwamba kupata medali kunaipa pia nchi sifa nzuri.

Naye mwanariadha, Alphonce Simbu, alisema kuwa ni vema maandalizi ya kushiriki michezo hiyo yakaanza mapema ili kuwaweka tayari kwenda kushindana.

Mwenyekiti wa Wanawake wa Michezo Kanda ya Tano, Irene Jackson, alisema kuwa wanamichezo ya sasa hivi wamekosa uzalendo tofauti na waliokuwa zamani kwa sababu ya kuangalia maslahi binafsi.

"Wanamichezo wa sasa ukiwaita kushiriki mashindano, kwanza anaanza kukuuliza atalipwa kiasi gani cha fedha, wakati anatambua michezo hiyo ni ya riadhaa," Irene alisema.

Kiongozi huyo aliwataka wanamichezo wastaafu kuendelea kutoa ushauri na kuwajenga chipukizi ili wawe tayari kuiletea nchi heshima kupitia Michezo ya Olimpiki inayokuja.

Habari Kubwa