Zanzibar Heroes yapata msaada

06Dec 2019
Na Mwandishi Wetu
ZANZIBAR
Nipashe
Zanzibar Heroes yapata msaada

KATIKA kuhakikisha inakwenda kufanya vizuri kwenye mashindano ya Kombe la Chalenji mwaka huu, Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF), imetoa kiasi cha Sh. milioni tano kwa Timu ya Soka ya Zanzibar (Zanzibar Heroes), imeelezwa.

Mashindano ya Kombe la Chalenji kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati yataanza kesho jijini Kampala na Zanzibar Heroes itaanza kampeni ya kuwania ubingwa huo Jumapili kwa kuwavaa Sudan.

Afisa Uhusiano wa ZSSF, Juma Mmanga, alisema kuwa mchango huo ni kwa ajili ya kuisadia Zanzibar Heroes katika mahitaji yake muhimu wakati wakiwa Uganda katika michuano hiyo.

Rais wa Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF), Seif Kombo Pandu, alisema kuwa, timu hiyo inahitaji hamasa zaidi kutoka kwa Wazanzibar ili ifanye vizuri katika michuano hiyo ambayo mwaka huu inashirikisha timu tisa.

Pandu alisema kuwa wanaishukuru ZSSF kwa mchango huo na kuongeza kwamba utakwenda kusaidia mahitaji ya wachezaji wao, ambao tayari wapo Uganda kwa lengo la kuwania kikombe hicho.

Habari Kubwa