Jela maisha kunajisi mtoto

06Dec 2019
Joctan Ngelly
KIGOMA
Nipashe
Jela maisha kunajisi mtoto

MAHAKAMA ya Wilaya Mkoa wa Kigoma, imemhukumu mkazi wa Kijiji cha Kalenge Wilaya ya Uvinza, Dastan Elia (40), kutumikia kifungo cha maisha jela kwa kumnajisi mtoto mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi saba.

Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu wa Mahakama hiyo, Eva Mushi, baada ya upande wa mashtaka kuthibitisha kosa hilo pasipokuacha shaka.

Hakimu Mushi alisema mahakama inatoa adhabu kali dhidi ya mshtakiwa huyo ili liwe fundisho kwake na kwa watu wengine wenye tabia ya kikatili kwa watoto kama yake.

Alisema upande wa mashtaka ulipeleka mashahidi wanane pamoja na vielelezo viwili ambavyo vilithibitisha kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo.

Aidha, alisema Julai 5 mwaka huu majira ya asubuhi katika kijiji cha Kalenge Wilaya ya Uvinza Mkoa wa Kigoma, mshtakiwa alimbaka mtoto huyo na kumsababishia maumivu sehemu zake za siri.

Alisema siku ya tukio hilo watoto walikuwa wakicheza mshtakiwa huyo aliwafuata na kuwafukuza, na baada ya kuwafukuza walitawanyika na baada ya kutawanyika mshtakiwa aliingia ndani ya nyumba na kumfanyia kutendo hicho cha kikatili mtoto huyo msichana.

Hakimu huyo alisema wakati mshtakiwa huyo anaendelea kumfanyia kitendo hicho, alifika dada wa mtoto huyo mwenye umri wa miaka 5 na kushuhudia, na baada kuona alikimbia kwa jirani na kuwapa taarifa.

Alisema jirani aliwaita majirani wengine na kwenda kumchukua mtoto huyo kumpeleka kituo cha Polisi Kazuramimba na walipofika walipewa fomu ya PF3 kisha kumpeleka Zahanati ya Kazuramimba na daktari alipomfanyia uchunguzi, alibaini kufanyiwa ukatili huo.

Hakimu Mushi alisema alisikiliza kesi hiyo pande zote na kugundua kuwa upande wa mshtaka umethibitisha kosa hilo pasipokuacha shaka, hivyo mshtakiwa umetiwa hatiani, na kumpa fursa mshtakiwa kujitetea.

Mshtakiwa alijitetea kuwa anaomba mahakama hiyo impunguzie adhabu kwa kuwa ni kosa lake la kwanza.

Hakimu Mushi alitupilia mbali utetezi huo na kusema kitendo alichokifanya ni cha kikatili, hivyo kumhukumu kwenda gerezani maisha.

Awali akisoma hati ya Mashtaka Wakili wa Serikali, Edina Makala, alidai Julai 5, mwaka huu majira ya asubuhi katika kijiji cha Kalenge Wilaya ya Uvinza, mshtakiwa alimnajisi mtoto huyo.

Habari Kubwa