Serikali yarekebisha kanuni uwekezaji, gharama zafyekwa

06Dec 2019
Na Mwandishi Wetu
MOROGORO
Nipashe
Serikali yarekebisha kanuni uwekezaji, gharama zafyekwa

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mussa Sima, amesema serikali imefanya mapitio ya Kanuni ya Tathmini ya Athari kwa Mazingira ili kurahisha uwekezaji nchi.

Akizungumza na wafanyabiashara na wawekezaji katika mkutano  wa kushauriana baina yao na serikali mkoani  Morogoro juzi, Sima alisema gharama za kulipia vibali zimepungua na idadi ya siku pia imepungua kutoka siku 145 za awali hadi siku 95.

“Ndugu zangu, marekebisho haya yote yanayofanywa na serikali, yanalenga kurahisisha mchakato wa tathmini ya athari kwa mazingira na kurahisisha uwekezaji nchini.

"Mfano, awali gharama kwa vituo vya mafuta zilikuwa zaidi ya Sh. milioni 10 lakini kwa sasa gharama hizi zimepungua hadi kufikia Sh. milioni nne na nyingine Sh. milioni mbili," alifafanua.

Naibu Waziri huyo alisema ofisi yake pia inaandaa kanuni za wataalamu elekezi wa mazingira ili kurahisisha uwekezaji kwa kuwa miradi yote kwa kuwa ni lazima ipate cheti kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC).

"Tangu tumefanya mapitio ya kanuni zetu, malalamiko kutoka kwa wawekezaji yamepungua kwa kiasi kikubwa sana," alisema.

Sima alitumia nafasi hiyo kuwakumbusha washiriki wa mkutano huo kuwa mabadiliko ya tabianchi ni tatizo kubwa duniani.

Alitoa rai  kwa  umma wa Watanzania kupanda miti kwa wingi kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.

Aliwaagiza wawekezaji, hasa wenye viwanda kuhakikisha wanaanzisha vitalu vya miche katika maeneo yao na kusisitiza kuwa ukaguzi wa masuala ya mazingira katika maeneo yao utaanzia hapo.

Mkutano huu ulilenga  kusikiliza na kutatua matatizo ya uwekezaji na utaendelea katika mikoa ya Pwani na Dar es Salaam. Mawaziri 13 na manaibu wao wanashiriki mkutano huu.

Habari Kubwa