Mbinga wahimizwa kuanzisha viwanda

06Dec 2019
Felix Andrew
Nipashe
Mbinga wahimizwa kuanzisha viwanda

SERIKALI wilayani  Mbinga Mkoa wa Ruvuma, imeeleza kwa sasa itatoa  kipaumbele kwa waombaji wa mikopo wenye mwelekeo wa kuanzisha viwanda  ili  kujenga uchumi wa viwanda  na kuongeza ajira.

Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Cosmas Nshenye

Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa wilaya hiyo, Cosmas Nshenye, wakati wa ufunguzi wa semina ya wazalishaji, wasindikaji na wauzaji wa bidhaa za chakula na vipodozi.

Nshenye alisema mikopo hiyo inayotolewa na Halmashauri ya Wilaya  kwa makundi ya vijana na wanawake haina riba, na kwa sasa  watakaopewa kipaumbele ni wale ambao wameitikia wito wa kuanzisha viwanda vya kusaga kahawa, watengenezaji wa batiki, wazalishaji wa sembe na bidhaa nyingine mbalimbali.   

“Walioitikia wito wa kujenga uchumi wa viwanda kwa kuanzisha viwanda tunawapongeza kwani tuna imani ajira zitaongezeka na  Kauli ya ‘Mbinga Mbingun’ itazidi kujidhihirisha kutokana na mafaniko yatakayotokana na viwanda,” alisisitiza.

Alisema pamoja na jitihada hizo za  wazalishaji za kuanzisha viwanda, pia wazalishaji wanapaswa kuzalisha bidhaa kwa kuzingatia viwango ili kuwa na uhakika wa ubora na bidhaa wanazozizalisha pamoja na uhakika wa soko ndani na nje ya wilaya hiyo.

Alisema fursa  ya elimu inayotolewa na Shirika la Viwango la Taifa (TBS) ni muhimu kwa wazalishaji kuizingatia kwani mbali na elimu hiyo inayotolewa bure, pia wajasiriamali hupatiwa huduma ya uthibitishaji wa ubora wa bidhaa bure kwa miaka mitatu ya mwanzo.

Akizungumzia kundi maalumu la wasindikaji wa pombe za kienyeji, ameiomba TBS kuangalia namna ya kuwawezesha wasindikaji pombe za kienyeji wanafikia viwango vinavyokubalika ili bidhaa zao zikidhi matakwa ya viwango na  kukubalika katika masoko ya ndani na nje ya nchi hususan katika soko la Afrika Mashariki.

Awali Kaimu Mkurugenzi wa Udhibiti Ubora na Meneja wa Utafiti na Mafunzo, Hamisi Sudi, akimkaribisha Mkuu wa Wilaya kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dk. Athuman Ngenya, alisema, Shirika litaendelea kutoa elimu ya viwango kwa Watanzania wote lengo kuu likiwa ni kuwa na uwelewa wa pamoja wa masuala ya viwango na ubora wa bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi na zile zinaingizwa kutoka nje nchi.

Naye mkuu wa Wilaya ya Songea,  Palolet Mgema, akifungua semina, Songea alisema  imefanyika katika kipindi muafaka kwani wafanyabiashara na wazalishaji walikuwa wakiisubiri kwa hamu ili kujua ni taratibu zipi za kufuatwa baada ya mabadiliko ya Sheria  ya fedha ya Mwaka 2019.

Habari Kubwa