Mahakama yataka taarifa Magereza ofisa NIDA kutofika

06Dec 2019
Hellen Mwango
Nipashe
Mahakama yataka taarifa Magereza ofisa NIDA kutofika

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imeuagiza upande wa utetezi kufuatilia taarifa za ugonjwa wa mshtakiwa wa tatu ambaye ni Ofisa Usafirishaji wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), George Ntalima, kwa maofisa Magereza kutokanana na kutofika mahakamani mara ya pili.

Kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya kusomwa maelezo ya awali mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Salum Ally.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Ladslaus Komanya, alidai kuwa kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya washtakiwa kusomewa maelezo ya awali.

Komanya alidai kwa kuwa mshtakiwa wa tatu hajafika mahakamani, Jamhuri inaomba wakili wa utetezi kuieleza mahakama mahali alipo mteja wake.

Wakili wa utetezi, Tuli Kaundime, alidai mshtakiwa huyo ni mgonjwa anasumbuliwa na majipu yaliyosababisha homa kali ndiyo sababu ya kushindwa kufika mahakamani.

Alidai afya ya mshtakiwa huyo imedhorota na kuiomba mahakama kupanga tarehe nyingine ya kutajwa.

Wakili Komanya alidai wakili wa mshtakiwa alitakiwa kutoa taarifa hiyo ikiambatanishwa na taarifa rasmi kutoka Magereza ili ijulikane kama anapatiwa matibabu au amepumzishwa.

Alidai kwa ajili ya kutenda haki kwa washtakiwa wengine, wakili huyo alete uthibitisho wa ugonjwa na sababu za kutompeleka mahakamani.

Akijibu hoja hiyo, Kaundime alidai mteja wake yupo mahabusu chini ya uangalizi wa Magereza hivyo, si sahihi kupeleka taarifa za ugonjwa au kueleza alipo mshtakiwa wakati wanafahamu yupo kwenye mikono salama ya Magereza.

Alidai wanaopaswa kutoa taarifa hiyo ni Magereza.

Hakimu Ally alisema ni wajibu wa upande wa mashtaka kupata taarifa za mshtakiwa huyo kutoka Magereza.

Hata hivyo, aliutaka upande wa mashtaka kuwasiliana na Magereza ili kupata taarifa za mshtakiwa huyo na kuieleza mahakama maendeleo yake.

Hakimu Ally aliahirisha kesi hiyo hadi Desemba 19, mwaka huu, kwa ajili ya kuwasomea washtakiwa maelezo ya awali.

Wengine kwenye kesi hiyo ya uhujumu uchumi ni aliyekuwa Mkurugenzi wa NIDA, Dickson Maimu, Meneja Biashara wa NIDA, Avelin Momburi; Ofisa Usafirishaji, George Ntalima; Xavery Silverius maarufu kama Silverius Kayombo na Mkurugenzi wa Sheria NIDA, Sabina Raymond.

Maimu na wenzake wanakabiliwa na mashtaka 55 yakiwamo ya kutakatisha fedha na kuisababishia serikali hasara ya Sh. bilioni 1.175.

Kati ya mashtaka mapya 55 waliyosomewa washtakiwa hao, yapo ya kuisababishia serikali hasara ya Sh. bilioni 1.175 ; utakatishaji fedha; kughushi; kuwasilisha nyaraka za uongo ili kumdanganya mwajiri wao; kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu; matumizi mabaya ya madaraka na kuongoza genge la uhalifu.

Hata hivyo, Maimu, Ntalima na Silverius wamerudishwa rumande kutokana na mashtaka yao kutokuwa na dhamana huku Momburi na Raymond wakiwa nje kwa dhamana.

Habari Kubwa