Mashinji aanika barua ya msimamizi uchaguzi

06Dec 2019
Hellen Mwango
Nipashe
Mashinji aanika barua ya msimamizi uchaguzi

KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Vincent Mashinji, anayekabiliwa na wenzake wanane na kesi ya uchochezi, amedai mahakamani kuwa barua ya msimamizi wa uchaguzi ilielekeza viapo na barua zitatolewa kwa wawakilishi wa mawakala.

Kadhalika, amedai kuwa kwa mujibu wa barua hiyo, wawakilishi wote baada ya kupokea nakala za viapo na barua watoe kwa mawakala.

Dk. Mashinji ambaye ni mshtakiwa wa sita alitoa madai hayo jana wakati akihojiwa na Jamhuri dhidi ya ushahidi wake mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Thomas Simba, anayesikiliza kesi hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.

Akihojiwa na Wakili wa Serikali, Jacqueline Nyantori, mshtakiwa huyo alidai kuwa alianza kazi akiwa Katibu Mkuu Chadema Machi 12, 2016.

"Barua ya msimamizi wa uchaguzi Kinondoni, ilielekeza wawakilishi wa mawakala kuchukua nakala za viapo na barua kwa ajili ya kuwapatia mawakala," alidai Dk. Mashinji.

Alidai kuwa katika barua hiyo ya msimamizi, hakuona maelekezo ya kufuata nakala za barua kwa maandamano na kwamba aliekeleza mawakala watapewa.

Naye shahidi wa saba, Halima Mdee, alidai mahakamani kuwa Februari 16, 2018 alisafiri kutoka Dodoma mpaka jijini Dar es Salaam na kwamba alikwenda kwenye viunga vya kufungia kampeni Kinondoni.

Alidai kuwa kutokana na hali ya afya yake haikuwa nzuri, alipanda jukwaani akasalimia na kumtakia heri ya uchaguzi mgombea Salum Mwalimu.

Alidai kuwa aliondoka saa 11:15 kwenda nyumbani kwake Mbweni jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kujiandaa kwenda kwenye matibabu nchini Afrika ya Kusini.

"Nilisafiri kwenye matibabu lakini siku niliporudi niliwakuta maafande wananisubiri Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere katika ukumbi wa VIP, walinikamata wakanipeleka Kituo Kikuu cha Polisi," alidai Mdee.

Alidai kuwa kuhusu kauli ya vichinjio, ilikuwa ina maana ya kwenda kupiga kura kuichagua Chadema na kumgalagaza Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais John Magufuli na wafuasi wake.

"Watu wa mjini tunafahamu kama kichinjio ni kadi ya kupigia kura kwa hiyo haina maana nyingine," alidai Mbunge huyo wa Kawe.

Mbali na Dk. Mashinji na Mdee  washtakiwa wengine ni Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu;  Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche; Mbunge wa Kibamba, John Mnyika; na  Mbunge wa Bunda, Ester Bulaya.

Pia wamo Mbunge wa Iringa Mjini,  Peter Msigwa; na Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko.

Washtakiwa hao kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 13, ikiwamo kula njama,  kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendaji jinai kati ya Februari Mosi na 16, 2018, Dar es Salaam.

Kesi inaendelea leo kusikilizwa ushahidi wa utetezi.

Habari Kubwa