Kaseja atemwa Kilimanjaro Stars

06Dec 2019
Somoe Ng'itu
Nipashe
Kaseja atemwa Kilimanjaro Stars
  • ***Nyota 22 waondoka kwenda kusaka ubingwa wa mashindano hayo unaoshikiliwa na ...

KATIKA hali ya kushangaza, aliyekuwa kipa chaguo la kwanza wa Timu ya Taifa (Taifa Stars), Juma Kaseja, ameachwa katika kikosi kitakachoshiriki mashindano ya Kombe la Chalenji ambayo yanatarajiwa kufanyika kuanzia kesho Desemba 7 hadi 19, mwaka huu jijini Kampala, Uganda.

Baada ya Kaseja kuachwa, magolikipa watatu waliobakia kwenye kikosi cha Kilimanjaro Stars chenye wachezaji 22, kilichoondoka nchini jana kwenda katika mashindano hao ni pamoja na Aishi Manula wa Simba, Metacha Mnata (Yanga) na David Kisu, ambaye anaidakia Gor Mahia ya Kenya.

Kaseja alikuwa ni mmoja wa wachezaji waliokuwa kwenye kikosi hicho kinachoongozwa na Kocha, Juma Mgunda, Suleiman Matola na Zuberi Katwila, waliofanya kikamilifu hadi mazoezi ya mwisho ya kikosi hicho yaliyofanyika jana asubuhi.

"Mimi siwezi kusema ni kwa nini nimeachwa, wenye nafasi nzuri ya kulizungumzia uamuzi huo ni wakubwa (benchi la ufundi) wenyewe, ila hadi kwenye mazoezi ya mwisho leo (jana), asubuhi nilikuwepo," alisema Kaseja, ambaye alisimama langoni katika mechi zote ambazo Taifa Stars imesheza na hatimaye kukata tiketi ya kushiriki fainali zijazo za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN).

Nyota wengine walioachwa katika kikosi hicho ni pamoja na Iddi Suleiman "Nado", Salum Aboubakar "Sure Boy", Frank Domayo na Shabani Chilunda.

Mgunda alisema kuwa amelazimika kuwaacha wachezaji hao kwa sababu ni majeruhi na wanahitaji kupata muda zaidi wa kupona ili taifa na klabu zao ziwatumie hapo baadaye.

"Kubwa ambalo limetokea kwa vijana hawa ni kupata majeraha wakati wa mazoezi, Nado ameumia siku moja kabla hatujasafiri, Chilunda alikuja akiwa ameumia, mchezaji wangu mkongwe, nahodha wangu, Kaseja alipata maumivu mguu wake wa kulia, madaktari wameshauri akafanyie vipimo na matibabu yaanze haraka, tutamhatarisha tukiendelea kumtumia," alisema Mgunda.

Aliongeza kuwa kikosi chake kimejiandaa vizuri kwenda kupambana na kusaka matokeo mazuri ili kulinda heshima ya nchi.

"Ni jukumu zito ambalo tumepewa na Watanzania, tunakwenda kushindana, katika ukanda wetu ni mashindano makubwa, vijana wako tayari, yoyote tutakayekutana naye ni mshindani wetu," alisema Mgunda.

Naye beki wa timu hiyo, Bakari Mwamnyeto, amesema kuwa wachezaji wanaahidi wanakwenda kushindana ili kurejea na ubingwa.

"Hii ni mara yangu ya kwanza kushiriki mashindano haya ya Chalenji, tumejiandaa vizuri, tunaenda kusaka ushindi, tunawaahidi mambo mazuri, " alisema beki huyo anayeichezea Coastal Union.

Wachezaji wengine wa Kilimanjaro Stars waliosafiri jana ni pamoja na Juma Abdul, Nickson Kibabange, Gadiel Michael, Mwaita Gereza, Mohammed Hussein "Zimbwe Jr", Bakari Mwamnyeto, Kelvin Yondani, Baraka Majogoro, Jonas Mkude, Zawadi Mauya, Mzamiru Yassin, Hassan Dilunga, Cleofas Mkandala, Paul Nonga, Miraji Athumani, Eliuter Mpepo, Kikoti Lucas na Rashid Chambo.

Kilimanjaro Stars itaanza kampeni ya kuwania ubingwa huo keshokutwa kwa kuwavaa mabingwa watetezi Harambee Stars ya Kenya, halafu itacheza mechi yake ya pili dhidi ya Zanzibar hapo Desemba 10 na itamaliza hatua ya makundi kwa kuvaana na Sudan hapo Desemba 14, mwaka huu.

Habari Kubwa