Simba: Tulihitaji huduma ya Okwi

06Dec 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Simba: Tulihitaji huduma ya Okwi

BAADA ya aliyekuwa Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Aussems, kusema kuwa hakurudhia kuondoka kwa mshambuliaji Emmanuel Okwi, uongozi wa timu hiyo umeibuka na kusema mganda huyo alihitaji kupata changamoto mpya.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Haji Manara, alisema kuwa Okwi aliamua kuondoka klabuni hapo baada ya kupata "ofa nono" na si kuachwa na viongozi.

"Hakuna kiongozi wa Simba ambaye alipenda kumuacha Okwi, mwaka 2018 tulitaka kumwongeza mkataba ili umalizike mwaka 2021, lakini alikataa akasema, anahitaji amalize mwaka huu na anataka kwenda kutafuta changamoto nyingine, hivyo hivyo kwa Kotei (James) ambaye alipata "dili" la Kaizer Chiefs," alisema Manara.

Aliongeza kuwa pia klabu hiyo ilichelewa kufanya uamuzi wa kumtimua Aussems, ambaye alikuwa amewagawa wachezaji katika makundi mawili, jambo ambalo halikuwa na "afya" kwenye timu hiyo.

Kiongozi huyo alisema pia kocha huyo alikuwa ni mtu asiyependa kupewa ushauri, na wakati mwingine akitoa kauli za kuwakatisha tamaa baadhi ya wachezaji.

"Kuna mechi wenzake walimshauri amchezeshe Dilunga (Hassan), bahati nzuri tulishinda, baada ya mechi akasema Dilunga ndio nani na mchezaji mwenyewe alisikia, akaamua kuondoka na kesho yake akasusia mazoezi," Manara alisema.

Aliongeza kuwa mbali na kutolewa mapema kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu, Aussems, ameweka rekodi mbaya ya kufungwa mabao mengi ugenini katika michuano hiyo msimu uliopita.

Habari Kubwa