Ma-RC mtegoni wanafunzi 58,000 wakikosa sekondari

06Dec 2019
Paul Mabeja
DODOMA
Nipashe
Ma-RC mtegoni wanafunzi 58,000 wakikosa sekondari

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, amewaweka mtegoni wakuu wa mikoa, baada ya kuwataka kujenga vyumba vya madarasa 1,467 ndani ya siku 86 kuanzia jana.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo

Lengo ni kupata madarasa yatakayotumiwa na wanafunzi 58,699 (asilimia 7.73) waliofaulu mtihani wa darasa la saba mwaka huu, lakini wamekosa nafasi za kujiunga na kidato cha kwanza mwakani, kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa.

Katika taarifa yake ya uchaguzi wa wanafunzi wa kujiunga na kidato cha kwanza mwakani aliyoitoa kwa waandishi wa habari jana, Jafo alibainisha kuwa kati yao, wavulana ni 28,567 (asilimia 48.53) na wasichana 30,132 (asilimia 51).

Jafo alisema kutokana na hali hiyo, anaagiza wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya zilizobakiza wanafunzi, kukamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa ifikapo Februari 29 mwakani.

Ingawa waziri huyo hakutaja idadi ya vyumba vya madarasa vinavyohitajika, wanafunzi 58,699 ni sawa na madarasa 1,467 kwa uwiano wa wanafunzi wa 40 kwa kila chumba cha darasa.

Jafo pia aliagiza makatibu tawala wa mikoa na wakurugenzi wa halmashauri husika, wasimamie utekelezaji wa agizo hilo ili kuhakikisha wanafunzi wote waliobaki wanajiunga na kidato cha kwanza ifikapo Machi 2 mwakani.

Aliitaja mikoa yenye uhaba wa vyumba vya madarasa na idadi ya wanafunzi waliobaki kwenye mabano kuwa ni Arusha (4,739), Dar es Saalam (5,808), Iringa (3,480), Kigoma (12,092), Lindi (1695), Manyara (728), Mara (9,493), Mbeya (2,716), Pwani (2,918), Rukwa (686), Simiyu (6,616), Songwe (4,684) na Tanga (3,044).

"Wanafunzi wote hao watajiunga na masomo yao baada ya vyumba vya madarasa kukamilika," waziri huyo alisema.

Jafo alibainisha kuwa mikoa ya Dodoma, Geita, Kagera, Katavi, Kilimanjaro, Morogoro, Mtwara, Mwanza, Njombe, Ruvuma, Shinyanga, Singida na Tabora imewachagua wanafunzi wote waliofaulu kujiunga na kidato cha kwanza katika shule za sekondari za serikali.

Alisema baada ya uchaguzi kukamilika, wanafunzi 701,038, sawa na asilimia 92.27, wakiwamo wavulana 335,513 (asilimia 47.86) na wasichana 365,525 (asilimia 52.14), wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwezi ujao.

Jafo alifafanua kuwa kati ya waliofaulu, wamo wanafunzi wenye ulemavu 1,461, sawa na asilimia 0.19 (wavulana 777 na wasichana 684).

Jafo pia aliwataka walimu wote na watumishi katika idara ya elimu, kuacha kuweka vikwazo vyovyote kwa wanafunzi waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza,  ikiwamo kuwatoza michango ili kutekeleza kwa vitendo dhana ya elimu bila malipo.

Habari Kubwa