Kili Stars, Zanzibar Heroes msifanye makosa Cecafa

07Dec 2019
Mhariri
Nipashe
Kili Stars, Zanzibar Heroes msifanye makosa Cecafa

KIPENGA cha kufunguliwa kwa michuano mikongwe Afrika [Kombe la Chalenji] mwaka huu kinatarajiwa kuanza kupulizwa leo kwa wenyeji, timu ya soka ya Taifa ya Uganda (Cranes), kuwakaribisha-

-Burundi katika mechi ya ufunguzi ya kinyang'anyiro hicho itakayopigwa kwenye Uwanja wa Namboole jijini Kampala, Uganda majira ya saa 10 jioni.

Michuano hiyo ya Cecafa Chalenji inaheshima yake Afrika kwani ndiyo mikongwe zaidi ya soka barani humu kutokana na kuanza mwaka 1926 ikijulikana kama Kombe la Gossage hadi mwaka 1966, ilipobadilishwa na kuwa Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati kabla ya 1971 kubadilishwa na kuwa Cecafa Challenge.

Mechi hiyo Uganda dhidi ya Burundi inatarajiwa kutanguliwa na mchezo mwingine kati ya Djibouti dhidi ya Somalia, utakaochezwa kwenye uwanja huo huo, kuanzia majira ya saa nane mchana.

Hata hivyo, macho na masikio ya Watanzania yanatarajiwa kuelekezwa zaidi uwanjani kesho watakati timu zao mbili za Taifa, Kilimanjaro Stars ya Tanzania Bara na Zanzibar Heroes ya Tanzania Visiwani, zitakaposhuka dimbani kwa nyakati tofauti.

Kilimanjaro Stars itashuka dimbani kupepetana na mabingwa watetezi, Harambee Stars ya Kenya wakati Zanzibar Heroes itakuwa na kibarua kigumu dhidi ya Sudan.

Katika michuano hiyo ambayo washindi wawili kutoka katika kila kundi watatinga nusu fainali, Kundi A linaundwa na wenyeji Uganda, Burundi, Eritrea, Somalia na Djibouti wakati Kundi B mbali ya Kilimanjaro Stars na Zanzibar Heroes, pia zimo Kenya na Sudan.

Mbali na kuwania ubingwa, michuano hiyo inayoandaliwa na Baraza la Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa), inatarajiwa kutoa nafasi nzuri kwa timu za ukanda huu zilizofuzu Kombe la Mataifa Afrika kwa Wachezaji wa ndani (CHAN), kujiandaa na mashindano hayo yatakayofanyika Aprili mwakani.

Hivyo ni matarajio yetu kuona Kili Stars, mabingwa wa 1975, 1994 na 2010 ama Zanzibar Heroes walioutwaa ubingwa huo mwaka 1995, timu mojawapo kati ya hizo ikirejea na taji hilo linaloshikiliwa na Harambee Stars kwa sasa.

Tunatambua haitakuwa michuano rahisi hasa kwa kuzingatia Harambee Stars, watataka kulitetea taji hilo, lakini pia wakipania kulipa kisasi kwa Tanzania ambayo iliwatoa kwenye michuano ya kuwani kufuzu CHAN Agosti mwaka huu.

Aidha, vita ya kuutwaa ubingwa huo haipo kwa Kenya na timu hizo za Tanzania pekee, bali pia tunatambua uwapo wa timu imara ya Uganda kutoka Kundi A, ambo ni mabingwa wa kihistoria wa michuano hiyo tangu mwaka 1971, wakiwa wameutwaa mara 14, wakifuatiwa na Kenya mara saba na kisha Ethiopia ambayo imejitoa kutokana na kukabiliwa na ukata ikiwa imeubeba mara nne.

Lakini hilo halitutii hofu kwani tunaamini, Kilimanjaro Stars ikiwa chini ya Kocha Juma Mgunda itaandika historia mpya kwa kuifikia Ethiopia kwa kuutwaa ubingwa mara ya nne na kama hilo likishindikana, basi Hemed Morocco ataiongoza vema Zanzibar Heroes na kuokoa jahazi kwa kurejea na taji hilo nchini.

Mbali na matarajio hayo, lengo letu ni kuona wachezaji wa Kilimanjaro Stars na wale wa Zanzibar Heroes wakionyesha uwezo mkubwa uwanjani ili kutoa wigo mpana kwa Kocha wa Taifa Stars, Etienne Ndayiragije kuchagua nyota watakaounda kikosi chake.

Katika michuano hii ya Cecafa, Ndayiragije atakuwa nchini Uganda kama mshauri wa makocha wa timu hizo mbili za Tanzania, lakini pia akilenga kuangalia wachezaji watakaounda kikosi cha Taifa Stars, hivyo ni wakati wa kila mmoja atakayepata nafasi kuonyesha uwezo wake ili kumshawishi kocha huyo wa timu ya taifa.

Hivyo, wakati wachezaji wakitekeleza wajibu huo, mashabiki, wadau wa soka na Watanzania kwa ujumla, hawana budi kuungana nazo nchini Uganda kuzishangilia na wale watakaoshindwa dua na maombi yao ni muhimu sana ili timu hizo za Tanzania ziweze kufanya kweli na kurejea na taji hilo ambalo kwa mara ya mwisho kubaki hapa nchini ilikuwa mwaka 2010 lilipobebwa na Tanzania Bara wakati huo ikiwa chini ya kocha Mdenmark, Jan Poulsen na michuano hiyo ikifanyika jijini Dar es Salaam.

Habari Kubwa